CCM Yang’aka Kada Wake Kushurutishwa Kuvua fulana ya Chama

Chama cha Mapinduzi kimelaani kitendo cha cha udhalilishaji kilichofanywa na Chacha Heche kumtaka mkazi mmoja wa Tarime kuvua fulana ya chama hicho aliyovua kama sharti la kumpa ajira.

Video iliyosambaa kwenye Mitandao ya kijamii inamuonyesha Chacha ambaye ni kaka wa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, John Heche akimlazimisha mzee huyo kuvua fulana aliyovaa yenye nembo ya CCM.

Taarifa iliyotolewa leo na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka imeeleza chama chake kusikitishwa na kitendo hicho hasa katika kipindi hiki ambacho mwenyekiti wake Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akionyesha nia ya kuliunganisha taifa kupitia maridhiano.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi na Uenezi wa Chadema John Mrema amesema jambo hilo wameliona kwenye mitandao ya kijamii na wameagiza kupewa taarifa ya kina kutoka kwa viongozi wa chama hicho wilayani Tarime.

“Kinachofanyika ni propaganda na hakukuwa na sababu ya chama tena ngazi ya taifa kutoa taarifa hiyo.

“Hata hivyo na sisi tumeagiza katibu wetu wa Tarime atuletee taarifa za kina kuhusu tukio hili, ilikuwaje maana kipande kinachoonekana ni kidogo baada ya hapo tutakuja na taarifa yetu kama chama,” amesema Mrema.

Katika taarifa aliyoitoa Shaka amezitaka mamlaka husika kuchukua hatua kali za kisheria kwa unyanyapaa dhidi ya mtanzania yeyote kama ambavyo imeonekana kwa mzee huyo aliyetakiwa kuvua fulana ili apate ajira.

Amesema, “Tutakumbuka Rais Samia baada ya kushika hatamu alitangaza dira yake ya kuliongoza taifa. Dira hiyo inalenga maridhiano ambayo yanatuweka pamoja bila kuangalia itikadi ya mtu, alichofanyiwa mzee yule si kitendo cha utu.”


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments