Fumbo la Dk Bashiru lawagawa makada CCM na wachambuzi


 Dodoma. Kauli ya mbunge wa kuteuliwa, Dk Bashiru Ally, imewaibua wanachama na makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kwa hali ya mambo ilivyo, wengi wanaitafsiri kauli yake kuwa sawa na msemo: ‘Fumbo mfumbie mjinga, mwerevu atalifumbua.

Dk Bashiru anashambuliwa kutokana na kauli iliyoitoa katika mkutano wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata) uliofanyika mkoani Morogoro Novemba 17 mwaka huu.


Kiongozi huyo ambaye ni wa kwanza nchini kuwa Katibu Mkuu wa CCM na wakati huo huo Katibu Mkuu Kiongozi, akiwa katika mkutano huo, alisema mtandao huo si chombo cha kutoa shukrani kwa yeyote yule, bali ni chombo cha kudai haki na heshima.

Alisema sauti ya wakulima iwatishe aliowaita wanyonyaji na kama hawajafika kwenye hatua hiyo ya kuwa watu au kundi la kutisha wanyonyaji, bado watakuwa hawajafikia malengo.

“Hatutakuwa tofauti na mawakala wao wanaowapambana wakati mwingine kuwadanganya kwamba unaupiga mwingi,” alisema Dk Bashiru.


Tafsiri ya kauli yake kwa makada

Taarifa za ndani kutoka kwa makada wa CCM, zinasema kauli za Dk Bashiru, ambaye ni msomi bobevu wa sayansi ya siasa, hana tofauti na kauli zilizotolewa na aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kuhusiana na Serikali kukopa nje na kwamba iko siku nchi itapigwa mnada.

“Hivi ni vita havina tofauti na vile ya Ndugai. Tuwaachie wenye vita yao,” ni kauli ya mmoja wa watoa taarifa wetu.

Aliendelea kudokeza: ‘Fumbo mfumbie mjinga mwerevu atalifumbua.’ akimaanisha kauli ya Dk Bashiru kwenye mkutano wa Mviwata siyo ya ulimi kuteleza kulingana na nafasi za uongozi alizowahi kushika ndani ya CCM na serikalini na hata werevu wake mkubwa wa mambo kama msomi.

Dk Bashiru kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na alikuwa mkosoaji mkubwa kwenye masuala ya kisiasa na kiuchumi nchini.

Kauli ya mtoa taarifa hiyo, inaungwa mkono na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie aliyesema licha ya Dk Bashiru kuwa na haki ya kutoa maoni, kilichopo ni kwamba anabanwa na nafasi za uongozi alizowahi kushika ikiwamo ya sasa ya ubunge.

“Maoni yake yako sahihi ya hamasa za watu kudai haki zao,” alisema Dk Loisulie, huku akiongeza kusema kuwa mifumo ya demokrasia, inawataka viongozi kuwajibika kwa wananchi wao.

Hata hivyo, Dk Loisulie alisema changamoto kwa Dk Bashiru ni nafasi zake za uongozi, kwanza ubunge wa kuteuliwa na Rais alionao sasa, ukatibu mkuu wa CCM na katibu mkuu kiongozi, nafasi alizowahi kushikilia. Alisema ukichukua nyadhifa hizo na ubobevu wake kielimu ni kama Dk Bashiru amefungwa kwa kukosa uhuru kama alivyokuwa zamani..

“Dk Bashiru ametoka kwenye taaluma alikokuwa na uwanja mpana wa kukosoa, maeneo aliyopo sasa ni tofauti na taaluma.

Hata hivyo, aliwataka makada wanaokosoa kauli ya Dk Bashiru kuwa na tahadhari.

“Pamoja na kushambulia wabakize maneno, hivi vijiti ni kupokezana. Huwezi kujua anaweza kuja kesho mwenyekiti mwingine akamchukua Dk Bashiru,” alisema.

Naye mchambuzi wa siasa na maendeleo, Bubelwa Kaiza alisema, watawala wa sasa wamefanya kosa kwani Serikali waliyoirithi haikutokana na ushindani, hivyo kuchangia watu wasio na uwezo kuingia serikalini.

“Hawana uwezo wa kushindana...sasa ukiwa kwenye mazingira ambayo yanaogopa ushindani, unaogopa sauti yoyote ya ushindani,” alisema.


Greyson Mgonja ambaye ni mchambuzi wa siasa, alisema Dk Bashiru hana kosa lolote na alitumia nafasi yake ya kutoa maoni.

“Maoni yake hayakuharibu dhana au wasifu wa mtu na hakutaja mtu, hakutaja ni aina gani ya kiongozi aliyemzungumzia, yeye alikuja na hoja na nilitegemea wale wanaomtaka ajiuzulu wajibu hoja badala yake wanaleta vihoja, wangejibu kwa hoja kile alichosema,” alisema .

Mgoja alisema, misingi ya CCM ambayo ilikuwa ikimtaka mwanachama aseme ukweli imewekwa nyuma badala yake, kumeibuliwa misingi ya kuwanyima uhuru wanachama kuzungumza.

Wahenga wanasema ni bora kujenga tabia ya kuweka akiba ya maneno kuliko hata chakula na fedha. Dk Bashiru hakuweka akiba ya maneno?

Je, makada wa CCM wanaomshambulia na wao wanachukua tahadhari ya kuweka akiba ya meneno?

Hayati Maalim Seif Sharif Hamad aliwahi kumueleza kiongozi mmoja waliyetofautiana naye, aweke akiba ya maneno. Pengine Dk Bashiru anaponzwa na kauli zake za nyuma alipokuwa Katibu Mkuu wa CCM.

Lakini wanaomshambulia Dk Bashiru kwa kauli yake, wanasukumwa na nini? Je, hawataki kuona mwenzao akitoa maoni yake kwa mfumo wa kukosoa?


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments