Majaliwa Atoa Ujumbe Wa Elimu Ya Bima Afrika


 Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amezitaka nchi barani Afrika kujenga uwezo kwa wataalam ikiwemo kujadili namna kuwajengea uwezo wa kitaalamu vijana na wanawake ili wapate ujuzi wa masuala ya bima na hifadhi ya jamii.

Aidha, amezitaka nchi hizo kuangalia namna ya kushirikiana katika sekta ya bima ili kupata namna nzuri ya kujikinga na majanga ikiwemo yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema hayo leo Jumatano Novemba 30, 2022 jijini Arusha wakati akifungua mkutano wa kwanza wa kimataifa wa mamlaka za usimamizi wa bima Afrika na hifadhi za jamii.


Majaliwa amesema ni muhimu wadau hao kujadiliana namna ya kuwajengea uwezo vijana na wanawake ili wapate ujuzi na uwezo wa masuala ya bima na hifadhi ya jamii.


"Jadilini namna ya kuwawezesha vijana na wanawake kwa nchi zetu za kiafrika, leo nimeambiwa jambo la kusikitisha kidogo kwa Afrika nzima tuna mtaalam mmoja tu mwenye uwezo mkubwa wa kuthaminisha majanga ya masuala ya ndege na yupo Afrika Kusini," amesema


Kuhusu elimu na matumizi ya bima, mamlaka na taasisi zinazohusika na usimamizi wa bima na hifadhi ya jamii zimetakiwa kuongeze juhudi ya utoaji wa elimu ya bima na hifadhi ya jamii zao kwani takwimu zinaonyesha wastani wa uelewa na matumizi ya bima kwa watu wengi barani Afrika bado ni ndogo.


Akizungumzia ushirikiano wa nchi hizo, Majaliwa ameaema nchi hizo zinapaswa kushirikiana katika maeneo mengi kwa ajili ya kukuza biashara na uchumi wa nchi zao, namna nzuri ya sekta ya bima itakavyoshirikiana kupata majibu ya namna nzuri ya kukinga majanga mbalimbali ikiwemo majanga ya mabadiliko ya tabianchi.


Kuhusu fursa zilizopo kwenye makubaliano ya eneo huru la biashara ya bara ya Afrika, amesema makubaliano hayo yameleta pamoja nchi 54 za Afrika na kuunda soko moja la watu takribani bilioni 1.4.

"Wataalamu wanakadiria iwapo tutaendeleza ushirikiano huu kwa kufanya biashara huru miongoni mwetu, bila shaka pato la Bara la Afrika litakua kwa wastani wa asilimia 6 hadi kufikia takriban dola 66.4 Trilioni kwa miaka 50 ijayo," amesema


Amesema ni vigumu kutenganisha hifadhi ya jamiii na bima kwani vyote vinajaribu kumlinda mtu na jamii dhidi ya majanga yanayoweza kutokea wakati wowote hivyo ni muhimu mifuko hiyo ione namna ya kuwapa kipaumbele wanawake, vijana, wazee na wakulima ambao wako katika mazingira magumu.


"Ni muhimu kuona uwezekano wa kujadili kwa mapana kuhusiana na namna ya mifuko ya hifadhi ya jamii inavyoweza kusaidia kuinua uchumi wa watu wetu na kusaidia kuondoa umaskini hasa kwa wanawake, vijana na wakulima," amesema


Kwa upande wake, Kamishna wa Bima nchini, Dk Baghayo Suqware amesema mkutano huo wa siku tatu umeshirikisha wasimamizi wa kampuni za bima na mifuko ya hifadhi ya jamii kutoka nchi 27 Afrika.


Amesema lengo ni kujadili mambo mbalimbali yatakayowezesha kuongeza upatikanaji wa huduma za bima barani Afrika, fursa zilizopo kwenye sekta ya bima katika nchi hizo na mahitaji ya kisera ili kukuza sekta hiyo.


Nyingine ni kuongeza kasi ya maendeleo barani Afrika kwa kupitia mageuzi ya sekta ya bima na hifadhi ya jamii na kuimarisha ushirikiano wa wasimamizi na watekelezaji wa masuala ya bima na hifadhi ya jamii.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments