Tanzania yajipanga soko la samaki maboko, parachichi China


 Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba nchini Tanzania amesema Serikali imeongeza bajeti katika Sekta ya Uvuvi hadi kufikia Sh60bilioni zitakazotumika katika ununuzi wa boti ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha mazingira ya kutumia fursa za soko la samaki za mabondo China.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba nchini Tanzania amesema Serikali imeongeza bajeti katika Sekta ya Uvuvi hadi kufikia Sh60 bilioni zitakazotumika katika ununuzi wa boti ikiwa ni jitihada za kuimarisha mazingira ya kutumia fursa za soko la samaki za mabondo China.


Mwigulu amesema katika fedha hizo, zaidi ya boti 240 zitanunuliwa na kupelekwa kwenye vikundi vya wavuvi waliokuwa wakivua kwa kutumia zana za kizamani.

Mwigulu ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Novemba 12, 2022 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipookuwa akieleza namna Serikali ilivyojipanga kuchangamkia fursa hiyo pamoja na soko la Parachichi.


Hatua hiyo inakuja baada ya kukamilika ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini China iliyoanza Novemba 2 hadi 4, mwaka huu kufuatia mwaliko wa Rais wa China, Xi Jinping.


“Mradi huo wa kuongeza zana za kisasa ni programu ya miaka mitatu ya kushughulika na sekta za uzalishaji, kama mwaka huu zitanunuliwa boti 200, mwaka ujao wa fedha zitanunuliwa 300 na kuongezeka tena mwaka mwingine wa fedha unaofuata,”amesema Mwigulu.


Kwa upande wa Zanzibar Mwigulu amesema walinunua boti za kutosha kwa ajili ya kufufua uchumi na tayari uzalishaji wa mazao ya samaki umeongeza chini ya fedha za Uviko-19.


Katika ziara hiyo, Rais Samia pamoja na mambo mengine alisaini mikataba 15 ikiwamo ya fursa za wakulima kuruhusiwa kuuza zao la parachichi na bidhaa za samaki hasa mabondo nchini humo.


Kuhusu Parachichi, Waziri Nchemba amesema kuna hatua kubwa zinachukuliwa kuanzia mbegu bora za kisasa, zitakazohakikisha mazao hayo yanakuwa ya viwango vinavyotakiwa nchini humo.


“Wizara ya Kilimo na ile ya Viwanda,Biashara  na Uwekezaji zinafanyia kazi hayo. Pia bajeti iliyopita, Serikali ilichukua hatua ya kuondoa baadhi ya kodi kwenye mazao ya parachichi na samaki kuanzia kwenye uzalishaji, uhifadhi na usafirishaji ikwemo vyumba vya ubaridi.


“Ndege yetu kwenda China itasaidia mazao yanayohitajika kusarifirishwa kwa haraka, kwa hiyo Serikali tayari imechukua hatua za maandalizi,”amesema Waziri huyo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments