Wadanyabiashara ndogondogo maarufa kama Wamachinga waliohamia Soko jipya jijini Dodoma wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira na miundombinu wezeshi ya kufanya biashara sokoni hapo na maeneo mengine nchini.
Wakizungumza wiki hii na Idara ya Habari-MAELEZO wamachinga hao wamesema kuwa uboreshaji wa mazingira ya kufanyia biashara kwa kujenga masoko ya wajasiriamali nchini kote umekuwa ni chachu kubwa katika kuleta maendeleo kwa wajasiriamali hao nchini.
Mmoja wa wajasiriamali hao, Bw. Yusuph Kasongele amesema kuwa kabla ya kuhamia katika soko hilo alikuwa anafanya biashara zake katika sehemu ambazo sio rasmi ikiwa ni pamoja na kufanya biashara mbele ya maduka ya watu kwa malipo jambo ambalo halikuwa sahihi.
“Tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi wa Soko hili la Machinga ambalo limetuepushie migogogoro mbalimbali,na pia kutuweka pamoja imetufanya kufanya kazi zetu kwa kufuata sheria na taratibu za nchi,” ameeleza Kasongele.
Aidha kwa upande wake Bi. Elina Msangi amesema Soko hilo limekuwa suluhisho kubwa kwa wamachinga hao kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya biashara katika maeneo ambayo sio rasmi na ambayo hayana mazingira mazuri ya biashara kwani jua na mvua vimekuwa vikwazo vikubwa kwao.
“Soko hili lina huduma mbalimbali za kijamii ambapo tumewekewa mpaka kituo cha kunyonyesha watoto.pia wametujengea kituo cha Polisi ambacho kinatuhakikishia usalama muda wote pamoja na stendi ya mabasi ambayo inaendelea kujengwa kwa hili tutapata wateja wa kutosha”ameongeza
Kwa upande wake Daniel Masawe ambaye ni mteja katika soko hilo amesema wanamshukuru sana Rais Samia kwa kuwajengea soko zuri sana ambalo kwa sasa limewarahisishia upatikanaji wa huduma zote katika sehemu moja.
“Kwa sasa huduma zote tunazipata sehemu moja hapa soko la Machinga iwe ni huduma za kibenki, mavazi ,chakula, stendi inajengwa hapa ya mabasi kwa hilo kwa kweli tunamshukuru sana Rais wetu kwa maendeleo haya”amesema.
Naye Afisa Biashara Mwandamizi wa Jiji la Dodoma Bi. Donatila Vedasto amesema soko hilo limeanza kufanya kazi Novemba 1, 2022 na mpaka sasa Soko hilo lina wajasiriamali 3,200, lina huduma za kifedha na huduma muhimu za jamii zikiwemo vyakula na vyoo na vyumba kwa ajili ya wakina mama kunyonyeshea watoto wao.
Soko hili limetengenezwa kutoa huduma masaa 24 ingawa kwa sasa tunatoa huduma kuanzia asubuhi mpaka saa nne usiku na limejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 9.5.
0 Comments