AFRIKA YAKUTANA KUJADILI HATMA YA PUNDA

 

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia) na baadhi ya Viongozi kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) na Shirika la Umoja wa nchi za Afrika linaloshughulika na tafiti na haki za wanyama (AU-IBAR) wakifurahia jambo muda mfupi kabla ya kuanza kwa Mkutano uliokuwa ukijadili hatma ya wanyama aina ya Punda uliofanyika leo (01.12.2022) jijini Dar-es-salaam.

Mkurugenzi wa Mtandao wa kutetea haki za wanyama kutoka Kenya Bw. Josphat Ngonyo akiwaeleza Waziri wa Mifugo na Uzalishaji wa wanyama kutoka Chad Dkt. Abderahim Awat (kushoto) na  Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kushoto) namna wanyama aina ya Punda wanavyotumika nchini kwake  muda mfupi kabla ya kuanza kwa Mkutano uliokuwa ukijadili hatma ya wanyama aina ya Punda uliofanyika leo (01.12.2022) jijini Dar-es-salaam. Wa pili kutoka kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Bw. Tixon Nzunda.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na Vuongozi na watendaji kutoka zaidi ya mataifa 20 wanachama wa Umoja wa Afrika na watendaji kutoka Shirika la Umoja wa nchi za Afrika linaloshughulika na tafiti na haki za wanyama (AU-IBAR) na Shirika linaloshughulikia haki za wanyama kazi (Brooke East Africa) wakati wa Mkutano uliokuwa ukijadili hatma ya wanyama aina ya Punda uliofanyika leo (01.12.2022) jijini Dar-es-salaam.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameziongoza nchi zaidi ya 20 wanachama wa Umoja wa  Afrika ambazo zimekutana leo (01.12.2022) jijini Dar-es-salaam kwa ajili ya kujadili hata ya wanyama aina ya punda wanaodaiwa kuwa kwenye hatari ya kutoweka.

Akizungumza katika Mkutano huo Mhe. Ulega amewataka wataalam kutoka katika nchi hizo kujadili kwa kina na kutoa mapendekezo ya kitafiti na kisayansi kuhusu njia zinazoweza kutumika kuwaokoa wanyama hao na kuziwasilisha ili zijumuishwe  katika sera na kanuni  kwa ajili ya utekelezaji.

“Kama tulivyofanikiwa katika kupiga vita biashara nyingine ambazo zilikuwa zikitupelekea kwenye kupoteza wanyama wetu basi mtafakari kama wataalam na kuja na tafiti za kisayansi zitakazotushawishi sisi watunga sera ili tuweke mkazo wa kupiga marufuku kama tulivyoweka kwa upande wa biashara ya meno ya Tembo” Amesisitiza Mhe. Ulega

Aidha Mhe Ulega amependekeza wanyama aina ya punda kujumuishwa kwenye kundi la viumbe waliopo hatarini kutoweka ili kuongeza nguvu ya jitihada zinazofanywa kwa ajili ya kuokoa hatma yao ambapo amesema kuwa hatua hiyo itafufua jitihada za kuongeza idadi ya wanyama hao.

“Lakini pia wakati mkijadili mnapaswa kujua kuwa pamoja na umuhimu wake kule vijijini wananchi wanashawishiwa kuuza punda wao kwa sababu ya umasikini hivyo wakati tunafikiria namna ya kudhibiti hali hii ya utowekaji wa Punda tufikirie namna ya kuwaelimisha na kuangalia njia mbadala kwa wanakijiji hao ili wasiwauze”Ameongeza Mhe. Ulega.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayeshughulikia Sekta ya Mifugo Bw. Tixon Nzunda amesema kuwa msisitizo mkubwa wa Tanzania katika mkutano huo ni kuueleza ulimwengu kuhusu hatua walizochukua katika kudhibiti hali ya kutoweka kwa punda ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku uuzwaji na uchinjwaji wa wanyama hao.

“Lakini jambo jingine tumeiambia dunia kuwa sisi kupitia mfumo wetu wa Sera tumeamua kulinda wanyama hawa kupitia eneo la ustawi wa wanyama lililopo kwenye mabadiliko ya sera ya Mifugo ya mwaka huu ambayo yanaendelea kufanyika” Amesema Nzunda.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa nchi za Afrika linaloshughulika na tafiti na haki za wanyama (AU-IBAR) Dkt. Nick Nwankpa amesema kuwa katika nchi zote za Afrika wanyama aina ya Punda wamekuwa na msaada mkubwa kwa jamii ikiwa ni pamoja na kusaidia katika shughuli zote za kiuchumi.

“Lakini pamoja na msaada huo, Punda wamekuwa wakichukuliwa kama wanyama kazi tu ambao wamesahaulika hata kwenye sera na kanuni mbalimbali zinazolinda haki za wanyama na kadri idadi kubwa ya watu inavyoongezeka ndipo idadi ya punda inavyopungua” Amesema Dkt. Nwakpa.

Akielezea sababu za kufanyika kwa mkutano huo nchini Tanzania Mwenyekiti wa Shirika linaloshughulikia haki za wanyama kazi (Brooke East Africa) Bw. Erick Kimani amesema kuwa hatua hiyo imetokana nchi hiyo kuwa ya kwanza kupiga marufuku biashara ya Punda ambapo amezitaka nchi nyingine za Afrika kuchukua hatua hiyo ili kuondoa hatari ya kutoweka kwa wanyama hao.

Mkutano huo unaofanyika kwa siku mbili jijini Dar-es-salaam umelenga kujadili kwa kina umuhimu wa wanyama aina ya punda kiuchumi na kijamii na unatarajia kuwa na maazimio yatakayosaidia kuwaondoa wanyama hao kwenye hatari ya kutoweka.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments