Ajali zatikisa familia, wanane wafariki dunia

Vifo vya wanandoa vinazidi kutikisa, safari hii watu wanane wakifariki kwa ajali mikoa ya Morogoro na Mbeya, huku wawili wakiwa ni mume na mke waliopata ajali Morogoro wakisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya.


 Hii ni ajali ya pili kuua wanandoa ndani ya siku tano katika barabara hiyo hiyo ya Morogoro-Iringa, baada ya wanandoa wawili ambao ni askari wa Jeshi la Polisi nchini, kufariki Desemba 20, 2022 katika eneo la Tanangozi mkoani Iringa.

Askari hao ambao ni Polisi katika mkoa wa Arusha, Noah Semfukwe (30) na Agnes Kiyeyeu (27) walipata ajali hiyo na kufariki dunia ikiwa ni siku nne tu tangu wafunge ndoa Jijini Arusha Desemba 17 na walikuwa wakisafiri kwenda mkoani Mbeya.


Katika ajali ya juzi mkoani Morogoro, waliofariki ni wanandoa ambao ni walimu Grayson Ngogo (50) na mkewe Janet Ruvanda (40), ambao pia walikuwa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Wengine waliofariki dunia katika ajali hiyo ni Owald Ruvanda (42) kaka wa mke wa Ngogo, Janet Haule (37) ambaye pia ni mwalimu na Festo Shoo aliyekuwa dereva wa gari aina ya Toyota Allion.


RPC Moro, DC wafunguka

Akizungumzia ajali hiyo, kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilim alisema ajali hiyo ilitokea Desemba 25, 2022 saa 6:45 usiku wa kuamkia juzi baada ya gari ya IT Toyota Allion namba 6954 kugongana na lori la mafuta.

“Gari hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Shoo wa kampuni ya Chosen Generation ya bandari ya Dar es Salaam. Hili gari lilikuwa linatoka bandarini Jijini Dar es Salaam kuelekea Tunduma Mbeya ili kulikabidhi kwa mmiliki wake,” alisema.

“Ilipofika hapa Iyovi liligongana na lori la mafuta lenye namba za usajili RAE 518 C na tela lRL 2686 Mercedes Benz. Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa gari dogo alikuwa akiendesha kwa mwendo mkali, mvua inanyesha na kuna kona kali.”

Kwa mujibu wa kamanda huyo, kutokana na mazingira hayo, dereva huyo ambaye ni miongoni mwa waliofariki alishindwa kuchukua tahadhari na kushindwa kulimudu akahama kutoka kushoto na kwenda upande wa kulia.

“Ukingalia kabisa katika hili eneo lote la Iyovi lina kona kali na mvua inanyesha, lakini dereva akawa anaendesha gari kwa mwendo mkali. Dereva wa lori alijitahidi sana kulikwepa lakini ikashindikana wakagongana uso kwa uso,” alisema.

Akizungumzia ajali hiyo, Mkuu wa wilaya ya Kilosa, Majid Mwanga, aliliagiza jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani, kuwachukulia hatua madereva wa magari yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi (IT) ambao wanabeba abiria.

Mwanga alisema ajali hiyo ni mbaya na imeleta simanzi kwa familia na jamii kwa ujumla kwa kuwa miongoni mwa waliofariki ni pamoja na wanandoa ambao walikuwa wakielekea kwao jijini Mbeya wakitokea Jijini Dar es Salaam.

“Hizi gari za IT zinazosafirishwa kutoka bandarini kwenda nje ya nchi zinapaswa kuwa na dereva tu na sio kubeba abiria, lazima tusimamie sheria. Askari wetu wa usalama barabarani wawe wanayakagua haya magari,” alisema Mwanga.

Walichokisema marafiki, OUT

Mmoja wa watu wanaofanya kazi na marehemu Ngogo, Magreth Kalonga alisema miili ya wanandoa hao ilihifadhiwa katika Hospitali ya Mtakatifu Kizito mkoani Morogoro lakini juzi usiku ilisafirishwa kuelekea Mbeya kwa ajili ya mazishi.

Alisema waliokufa kwenye ajali hiyo ni pamoja na familia moja ambayo ilihusisha wanandoa hao na shemeji wa mwanamume, wote walipanda gari la IT kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya kabla ya kupata ajali eneo la Iyovi mkoani Morogoro.

“Taratibu za mazishi ni kesho (leo), zitafanyika hapa hapa Mbeya walikokuwa wakiishi na kufanya kazi,” alisema mwanamke huyo ambaye pia ni mshauri wa wanafunzi katika Chuo cha Ualimu cha Mtakatifu Aggrey kilichopo mkoani humo.

Kalonga alibainisha kwamba Ngogo alikuwa akifanya kazi kama Makamu Mkuu wa chuo hicho wakati mke wake alikuwa mwalimu wa shule ya sekondari Legico na wawili hao wameacha watoto wawili na kusema msiba huo umewaumiza sana.

Kwa upande wake, Rais wa serikali ya wanafunzi wa OUT, Felix Lugeiyamu alithibitisha kwamba taarifa hizo ni za kweli na kwamba walikuwa ni wanafunzi wa chuo hicho katika tawi la Mbeya ambako walikuwa wanasoma shahada ya uzamili.

“Taratibu za mazishi zitakuwa chini ya familia ambapo tunasubiri kupewa taarifa kwamba yatakwendaje,” alisema Lugeiyamu huku Mkurugenzi wa Masomo ya Juu wa OUT, Profesa Magreth Bushesha akisema hakuwa na taarifa za vifo hivyo.


Ajali ya Mbeya ilivyoua watatu

Wakati ajali ya Morogoro ikigharimu maisha ya watu watano, wakiwamo wanandoa wawili, mkoani Mbeya, lori la mafuta aina ya Faw liliangukia gari dogo aina ya Toyota Vanguard na kusababisha vifo vya watu watatu.

Ajali hiyo ilitokea juzi Desemba 26, 2022 saa 7:30 mchana katika kijiji cha Ntokela wilaya ya Rungwe na kusababisha kifo cha dereva wa gari dogo, Ipyana Kyomo (59) ambaye ni mwalimu mstaafu na mmiliki wa Shule ya Msingi Heritage. Wengine waliofariki katika ajali hiyo ni Irene Kyomo (14), mwanafunzi wa kidato cha pili anayeingia kidato cha tatu katika Sekondari ya Centennial Christian iliyopo Mkuranga mkoani Pwani na Elizabeth Lucas (20), mfanyakazi wa kazi za ndani.


Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Benjamin Kusaga alisema jana kuwa gari hilo dogo lenye namba T103 DPZ lilikuwa likitoka Kyela kuelekea Mtwara wakati lori la mafuta namba T745 DPZ na tela T258 DRJ likitoka Dar es Salaam kuelekea Malawi.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, katika ajali hiyo watu wanne walijeruhiwa ambao ni Yunis Nyiti (51), Idrisa Mwende (30), Vanesta Amasha (12) na Elizabeth Mrope na kwamba waliopata ajali ni familia moja na rafiki yao mmoja.

Majeruhi watatu wamepelekwa hospitali ya misheni Igongwe kwa matibabu na miili ya marehemu imepelekwa Hospitali ya Mekandana na kwamba chanzo cha ajali ni dereva wa lori, Jimmy Benasusi kuendesha gari kwa mwendo wa hatari.

Chanzo Mwananchi

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments