Dk Tulia ametoa agizo hilo leo Alhamisi, Desemba 29, 2022 mara baada ya kupata malalamiko ya wakulima kuhusiana na kukosekana kwa mbolea na kulazimika kufanya ziara ya kushtukiza kwa baadhi ya mawakala ikiwepo Kampuni ya DRTC.
“Nimefika hapa kwa suala moja tu la mbolea, maana nimepata malalamiko ya wakulima kuwa mbolea hakuna na hapa nimefika kwa wakala wa kampuni ya DRTC ipo tena ya kutosha nahitaji wakulima wapatiwe,” amesema.
Dk Tulia ambaye pia ni mbunge wa Mbeya Mjini amesema kitendo cha wakulima wadogo kukosa mbolea huku wakubwa wakinufaika sio malengo ya Serikali.
“Serikali imetoa utaratibu wa ugawaji wa mbolea kwa wakulima, sasa nashangaa ninapo elezwa mbolea hakuna na wakulima wakiangaika hali ambayo sio busara, sasa suala la mifumo ambayo wakala unalalamikia nawasilisha serikalini cha msingi wakulima kuanzia sasa wapewe mbolea,” amesema
Mkulima Faustina Charles, mkazi wa Itezi Magharibi ameiomba Serikali kuingilia kati ili waweze kupata pembejeo kulingana na mahitaji kwani msimu wa kilimo unapita bila sababu.
“Mh nimefika hapa tangu saa 12.30 za asubuhi mpaka sasa saa 7.00 mchana sijapata mbolea na tangu muda huo ndani ya saa moja wanahudumiwa watu watatu na tunapohoji tunaelezwa mbolea imekwisha tusubiri mpaka Jumanne ya Januari 3,” amesema.
Kwa upande Wakala wa Mbolea wa Kampuni ya DRTC, Leonard Mpayo alikiri kuwepo kwa changamoto na kwamba mifumo ya uingizaji wa taarifa imechangia wakulima kutopata mbolea kwa wakati.
Wakati huo huo, Dk Tulia ameshiriki ujenzi wa vyumba sita vya madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika shule ya Sekondari ya Iganzo.
Chanzo Mwananchi
0 Comments