Kesi Ya Kina Mdee Yaahirishwa Hadi Machi 6

Mahakama Kuu imeahirisha kesi iliyofunguliwa na wabunge 19 wakipinga uamuzi wa Chadema kuwafukuza uanachama, baada ya wakili anayewakilisha Chadema, Peter Kibatala kuwa kwenye vikao vya Mahakama Kuu vya usikilizwaji wa kesi za jinai vinavyofanyika mkoani Mwanza.

Akizungumzia hatua hiyo leo Jumanne Desemba 6, wakili anayemwakilisha Halima Mdee na wenzake 18, Edson Kilatu amesema shauri hilo lilikuja Kwa ajili ya usikilizwaji na mahakama hiyo imepanga kusikiliza shauri hilo Machi 6 na 9, 2023.

"Wakili Kibatala aliomba udhuru na kutujulisha pamoja na mahakama yenyewe kutokana na sababu hiyo ya msingi mahakama hili imeridhia ihairishe shauri hili," amesema Kilatu.


Kilatu amesema sasa hivi mahakama inaenda likizo na baada ya likizo hiyo itaanza vikao vya mahakama Kuu vya usikilizwaji wa kesi za jinai hivyo shauri hilo imesogezwa mbele hadi Machi 6 na 9, 2023.

Kesi hiyo ipo mbele ya Jaji, Cyprian Mkeha ambapo Mbunge wa viti maalumu, Jesca Kishoa ataendelea  kuhojiwa  Machi 6 na 9,2023 na mawakili wa Chadema.

Wabunge hao wanapinga uamuzi huo kwa utaratibu wa Mapitio ya Mahakama (Judicial Review), wakidai kuwa walifukuzwa isivyo halali kwa kuwa hawakupewa haki ya kusikilzwa, hivyo wanaiomba mahakama hiyo itengue.

Wengine walioitwa kuhojiwa ni aliyekuwa mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee, aliyekuwa makamu mwenyekiti Bawacha, Hawa Mwaifunga, aliyekuwa Katibu Bawacha, Grace Tendega, na aliyekuwa mweka hazina Bawacha, Ester Matiko; Ester Bulaya na Cecila Pareso.

Mpaka sasa tayari wabunge watano wa Viti Maalumu wamehojiwa na mawakili wa Chadema kuhusiana na ushahidi wao waliowasilisha mahakamani hapo Kwa njia ya kiapo ni Hawa Mwaifunga, Grace Tendega, Nusrati Hanje, Cecilia Pareso na Kishoa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments