MAAFISA TARAFA WATAKIWA KUTUMIA VIZURI MUDA WA KAZI KUWAHUDUMIA WANANCHI


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akizungumza na Maafisa Tarafa wa Mikoa (hawapo pichani) wakati akifunga Mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji Maafisa hao yaliyofanyika katika Ukumbi wa Informatics Chuo Kikuu cha Dodoma.


Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Dkt. Edith Rwiza, akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi kufunga Mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji Maafisa Tarafa wa Mikoa yaliyofanyika katika Ukumbi wa Informatics Chuo Kikuu cha Dodoma.


Baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji Maafisa Tarafa wa Mikoa wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi (hayupo pichani) wakati akifunga mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Informatics Chuo Kikuu cha Dodoma.




Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Ramadhani Kailima, akitoa nasaha kwa Maafisa Tarafa wa Mikoa walioshiriki Mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji Maafisa hao yaliyofanyika katika Ukumbi wa Informatics Chuo Kikuu cha Dodoma.




Afisa Tarafa wa Elerai Wilaya ya Arusha, Bw. Titho Cholobi akitoa neno la shukrani kwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Ramadhani Kailima kwa niaba ya washiriki wa Mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji Maafisa Tarafa wa Mikoa yaliyofanyika katika Ukumbi wa Informatics Chuo Kikuu cha Dodoma.


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi (katikati) akifurahia jambo wakati akiagana na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bw. Ramadhani Kailima (Wa kwanza kulia) mara baada ya kufunga Mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji Maafisa Tafara wa Mikoa yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Informatics Chuo Kikuu cha Dodoma. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Dkt. Edith Rwiza.


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mafunzo ya kuwajengea uwezo kiutendaji Maafisa Tarafa wa Mikoa mara baada ya kufunga Mafunzo ya Maafisa hao yaliyofanyika katika Ukumbi wa Informatics Chuo Kikuu cha Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu-TAMISEMI, Bw. Ramadhani Kailima na kushoto kwake ni Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Dkt. Edith Rwiza.

……………………………

Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amewataka Maafisa Tarafa 48 waliohudhuria mafunzo ya kujengewa uwezo kiutendaji, kuutumia vizuri muda wa kazi katika kuwahudumia wananchi kama ambavyo Serikali imekusudia.



Bw. Daudi ametoa wito huo kwa Maafisa Tarafa hao jijini Dodoma, wakati akifunga mafunzo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI ili waendane na kasi ya utendaji kazi ya Serikali ya Awamu ya Sita.



Bw. Daudi amewataka Maafisa Tarafa kutotumia muda wa kazi katika mitandao ya kijamii wakati wana jukumu la msingi la kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi katika maeneo yao ya kazi.



Bw. Daudi ameongeza kuwa, ofisi yake imeshirikiana na TAMISEMI kuandaa mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Maafisa Tarafa, kwa kutambua kuwa maafisa hao ni kiungo muhimu kati Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na Taasisi za Umma.



“Ninyi ni kiungo kikubwa cha kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi, hivyo ukisikia Serikali inalaumiwa kwa kutotoa huduma bora kwa wananchi au kupongezwa kwa kutoa huduma bora ninyi Maafisa Tarafa mnahusika, na ndio maana tumeamua kuwapatia mafunzo ili mkatekeleze majukumu yenu kikamilifu,” Bw. Daudi amefafanua.



Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI amewataka Maafisa Tarafa kusimamia nidhamu katika Utumishi wa Umma kwa ngazi ya tarafa kwani Sheria inamtambua Afisa Tarafa kuwa ni mwakilishi wa Afisa Tawala wa Wilaya kwenye ngazi ya tarafa ambapo moja ya jukumu la Afisa Tawala Wilaya ni kuhakikisha mamlaka zote za Serikali kwenye ngazi ya wilaya zinatimiza majukumu ya kiutumishi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya utumishi wa umma iliyopo.



Naye, Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Edith Rwiza amesema, mafunzo kwa Maafisa Tarafa hao yametolewa kwa siku mbili yakilenga kuwajengea uwezo Maafisa Tarafa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora na endelevu kwa wananchi.



Akizungumza kwa niaba ya Maafisa Tarafa waliopatiwa mafunzo, Bw. Titho Cholobi ambaye ni Afisa Tarafa wa Elerai Wilaya ya Arusha amesema kuwa mafunzo waliyopatiwa yamewawezesha kuzaliwa upya kiutendaji na kuongeza kuwa, yeye binafsi mafunzo hayo yamemuwezesha kubaini mapungufu aliyokuwa nayo katika utendaji kazi wake.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments