Majaliwa ataja mikoa yenye changamoto zinazoletwa na mifugo

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa amebainisha mikoa 11 ya Tanzania inayokabiliwa na changamoto nyingi zinazosababishwa na mifugo ikiwamo migogoro ya wakulima na wafugaji, uharibifu wa vyanzo vya maji na misitu iliyohifadhiwa kisheria.

Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni pamoja na Morogoro, Iringa, Pwani, Lindi, Arusha, Manyara, Kagera, Katavi, Tabora, Tanga na Mwanza.

Akizungumza katika kikao kazi cha viongozi wa Serikali ya mkoani Morogoro leo Desemba 24, 2022, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kikao hicho kinachotokana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan yanayohusu kusimamia kwa karibu sekta ya mifugo ili kutatua changamoto hizo.


“Leo tunaona changamoto kubwa za wakulima na wafugaji zinazosabanisha mauaji, wanakatana mapanga, hata jana niliangalia kwenye runinga nikaona kuna mahali wakulima wanalalamika mifugo imeingia kwenye mashamba yao ya mpunga na kuharibu mazao,” amesema Majaliwa.

Amesema kutokana na hali hiyo, kila kiongozi anapaswa kuwajibika kwa kusimamia haki, usalama na kutoa elimu elimu kwa jamii ambayo kwa sasa imekuwa na roho ya kikatili.

Majaliwa amesema kutokana na migogoro hiyo ya wakulima na wafugaji, jamii imekuwa na chuki lakini pia kumekuwa na vitendo vya rushwa miongoni mwa viongozi ambao pia wamekuwa wakichochea migogoro hiyo.

“Polisi wenyewe sasa hivi wameanza kudhibitiwa na wananchi juzi juzi tu huko Malinyi ama Ulanga. Polisi walifungiwa ndani ya nyumba chini ya udhibiti wa wananchi, tukifika hapo hiyo haina tija, chombo cha ulinzi na usalama kinadhibitiwa na raia nini maana ya uwepo wake? Kwa nini imetokea hiyo? Wananchi wamechoka au sisi viongozi hatuwajibiki?” amehoji Majaliwa.

Amesema mkuu wa nchi anapoonesha kutoridhishwa na maeneo fulani, ni wajibu wa viongozi hao kuweka mpango mkakati wa pamoja wa kudhibiti changamoto za mifugo na kujua nini cha kufanya katika kukabiliana na changamoto hiyo.

Awali akitoa salamu zake, mkuu wa mkoa wa Morogoro, Fatuma Mwasa amesema yeye pamoja na viongozi wenzake wako tayari kupokea na kutekeleza maagizo na maelekezo yote yatakayotolewa na waziri huyo mkuu na Serikali kwa ujumla.

Amesema ujio wa Waziri huyo mkuu umeleta faraja kwa wananchi na viongozi na wananchi wa mkoa wa Morogoro.

Kikao hicho kimehusisha mkuu wa mkoa wa Morogoro Fatuma Mwasa, wakuu wa wilaya zote za mkoa huo, wenyeviti wa halmashauri, makatibu tawala wa wilaya, wakuu wa taasisi za umma ikiwemo Tawa na TFS, kamati za ulinzi na usalama za wilaya na wakurugenzi kutoka Wizara ya Kilimo na Mifugo.

Baadhi ya mawaziri walioambatana na Waziri Mkuu ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Anjela Kairuki, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, Naibu Waziri wa Ardhi, Ridhiwani Kikwete na Naibu Waziri wa Kilimo, Antony Mavunde.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments