Recent-Post

NTIBAZONKIZA HUYOOO!!! SIMBA SC, AJIUNGA NA KAMBI MWANZA

Mshambuliaji raia wa Burundi, Saido Ntibazonkiza rasmi amesajiliwa na Simba SC kwa kandarasi ya mwaka mmoja na nusu akitokea katika Klabu ya Geita Gold ya mjini Geita ambapo alisajiliwa kwa mkataba wa mwaka mmoja pekee akitokea Yanga SC.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Simba SC, imeeleza kuwa Uongozi wa Klabu hiyo umefika makubaliano ya kumsajili Mchezaji huyo mwenye uzoefu mkubwa akiwa amecheza Ligi mbalimbali ulimwenguni katika nchi za Ufaransa, Uturuki, Poland na Tanzania kwa zaidi ya misimu miwili.

Ntibazonkiza akiwa na Geita Gold FC alipachika wavuni mabao manne akitoa ‘assist’ sita, tayari amewasili jijini Mwanza kujiunga na Kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi ambacho kinajiandaa na mchezo wake wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara dhidi ya KMC FC utakaopigwa kwenye dimba la CCM Kirumba, Desemba 26 mwaka huu.

Usajili wa Ntibazonkiza unakuwa wa kwanza kwa Kikosi cha Simba SC katika dirisha dogo la usajili, huku Wekundu hao wa Msimbazi wakitoa taarifa ya kufanya usajili wao kwa umakini bila shinikizo kutoka mahali popote.


Post a Comment

0 Comments