RONALDO ATIMKIA SAUDI ARABIA

Nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo rasmi amekamilisha usajili wake na tayari amejiunga na Al Nassr FC ya Saudi Arabia kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Manchester United ya Uingereza ambapo alivunja mkataba wake kwa makubaliano ya pande mbili.

Al Nassr FC wamethibitisha kumsajili Nyota huyo mwenye mafanikio makubwa katika soka ulimwenguni huku ikielezwa kuwa mkataba wake utatamatika mwezi June 2025. Ronaldo ametajwa kupokea kitita cha fedha za kigeni ziadi ya £177M kwa mwaka, akiwa Klabuni hapo kwenye ukanda huo wa bara la Asia.

“Hii ni zaidi ya historia katika kufanya maboresho. Huu ni usajili ambao sio tu utaipa Klabu yetu msukumo wa kupata mafanikio makubwa zaidi bali hata kupata msukumo Ligi yetu, taifa letu na vizazi vijavyo, Wavulana na Wasichana kuwa mfano mzuri kwao. Karibu Cristiano Ronaldo kwenye nyumba yako mpya Al Nassr FC,” ameandika Ronaldo sanjari na Klabu hiyo kupitia mitandao yao ya kijamii.

Ronaldo aliondoka Manchester United kwa kuvunja mkataba kwa makubaliano ya pande mbili baada ya kutokea sintofahamu kufuatia mahojiano aliyoyafanya na Kituo kimoja cha Runinga huko nchini Uingereza, mahojiano yaliyoongozwa na Mtangazaji Piers Morgan, ambapo Ronaldo alinukuliwa akidaiwa kusema amesalitiwa na Klabu hiyo ya Old Trafford pia alidaiwa kutomuheshimu Kocha wa timu hiyo, Erik Ten Hag.

Ronaldo, alifunga mabao 145 katika michezo 346 akiwa Manchester United, kabla ya kujiunga na Juventus ya Italia baadae aliondoka Juventus na kurejea Old Trafford mwaka 2021 ikiwa ni miaka 11 baada ya kuondoka na kujiunga na Real Madrid ya Hispania.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments