Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 18 katika eneo la mradi huo uliopo katika bonde la mto Rufiji, Waziri wa Nishati, January Makamba amesema mpaka sasa ujenzi wa bwawa hilo umefikia asilimia 78.68 ambayo ni hatua ya awali ya kuanza kujaza maji na inategemewa kuchukua misimu miwili ya mvua iliyokamili.
"Wakati mradi unaanza kutekelezwa ili kujengwa handaki (tuta) katikati ya mto ni lazima maji yachepushwe kwa njia nyingine ili yaendelee mbele yakupe nafasi ya sehemu kavu kujenga handaki hili lenye urefu wa mita 700 lenye gharama ya Sh235 bilioni," alisema Makamba.
Ameongeza kuwa mageti ya kuziba mchepusho wa maji ya kujaza maji yamewasili na tayari yameshafungwa na ni miongoni mwa hatua tatu muhimu zilizofanyika katika utekelezaji wa mradi huo hivyo anaona fahari kuutangazia umma hatua hiyo.
"Kutokana na umuhimu na ukubwa wa mradi huo na umuhimu wa mradi kitaifa ishara ya mradi huu kwa malengo yetu na ndoto yetu kwa maendeleo na hatua hii ya kujaza maji kwenye bwawa itazinduliwa na kushuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan Desemba 22 mwaka huu siku ya Alhamis," amesema.
Amesema kuwa hatua hiyo inakwenda kujibu mijadala ya baadhi ya watu waliokuwa wakidhani kwamba mradi huo hautokamilika kwa muda uliopangwa lakini pia hata uwezekano wa kujaza maji utawezekana kutokana hali ya ukame inayoendelea.
Akifafanua dhana hiyo ya kupoteza muda, Makamba, alisema kuna aina mbili za kuzalisha umeme kwa kutumia maji, hatua ya kwanza maji yanakuja kwenye mto na yanatiririka moja kwa moja kwenye mitambo, yanajengewa eneo la kukusanywa alafu yanaendesha mitambo, mfano bwawa la Kihansi.
Alieleza namna nyingine ya miradi hiyo kuwa ni kujenga bwawa na kuyakusanya maji mengi alafu unayaingiza kwenye mitambo halafu unayazungusha na kuzalisha umeme, mafano Bwawa la Mtera.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco), Maharage Chande, amesema kuwa bwawa hilo linauwezo wa kuhifadhi lita bilioni 33.2 za maji na kama zikitumika na mitambo yote itaweza kuendesha mitambo kwa kipindi cha mwaka mmoja.
0 Comments