Ukomo Viti Maalumu Wapasua Vichwa Wanasiasa, Wadau

 
Kikosi kazi hicho kilichokabidhi taarifa yake Oktoba 21, mwaka huu kilipendekeza miaka 10 kuwa ukomo wa muda wa wanawake kuhudumu katika nafasi hizo, ili kutoa nafasi kwa wengine kuinuliwa.

“Utaratibu wa kuwa na viti maalumu vya wabunge, wawakilishi na madiwani wanawake uendelee, isipokuwa sheria ziboreshwe kuweka ukomo wa miaka 10 kwa mtu kuwa mbunge, mwakilishi au diwani wa viti maalumu vya wanawake.
“Uwakilishi huu uwe ni njia ya kupata uzoefu na kisha kupisha wanawake wengine wenye nia ya kuongeza ujuzi wa masuala ya siasa na uongozi,” inaeleza ripoti hiyo.

Hata hivyo, pendekezo hilo limewaibua wadau wa siasa na viongozi wakongwe, akiwemo Sophia Simba, aliyeeleza ugumu wa utekelezwaji wake.

Sophia, ambaye ni Waziri wa zamani wa maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, anasema alipokuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) alitaka mabadiliko hayo, lakini hakufanikiwa.
Ugumu unatokana na kile anachokieleza kuwa, wengi tayari ni wanufaika wa nafasi hizo, hivyo ukiibua mjadala huo unagusa maslahi yao.

“Wengi hawataki kusikia kwa sababu ni wanufaika, ukizungumza utagombana na watu kwa kuwa unagusa masilahi yao, lakini tukirejea kwenye msingi wa kuanzishwa kwa viti hivi ni kuwawezesha wanawake, haiwezekani kila siku wawezeshwe walewale.

“Tunaamini kwamba baada ya miaka 10 tayari unakuwa na uwezo wa kifedha na maarifa yatakayokuwezesha kupambana jimboni,” anafafanua Mbunge huyo wa zamani wa Viti Maalumu kupitia CCM.
Anasisitiza ukomo wa muda wa kushika nafasi hizo, utatoa nafasi kwa wengine wengi kunufaika nazo.

Anasema kama dhamira ya kuanzishwa kwake ilikuwa kuwawezesha wanawake, miaka 10 inatosha mtu kuwezeshwa, ni vema apishe wengine wawezeshwe.
“Watu wanang’ang’ania wakati vilianzishwa kuwawezesha wanawake, sasa wewe umeshawezeshwa pisha nenda jimboni ili uruhusu na wenzako wawezeshwe,” anasema.

Balozi Getrude Mongella, ambaye kwa muda mrefu amekuwa miongoni mwa vinara wa kutetea haki za wanawake anasema ni vema ukafanyika uchambuzi wa kina kabla ya utekelezwaji.
Balozi Mongella anasema msingi wa kuanzishwa kwa viti maalumu haukulenga muda gani mwanamke atakaa kwenye nafasi hiyo, bali kumwezesha mwanamke apate fursa ya kuonyesha vipaji vyake vyote.

“Siwezi kujadili ya kikosi kazi kwa sababu sikusoma, lakini kuhusu viti maalumu vilianzishwa kuwawezesha wanawake, hakukuwa na suala la muda gani wakae kwenye nafasi hizo, kwa hiyo suala halikuwa muda, lililokuwepo ni ulazima wa uwepo wake kama njia ya kuwawezesha wanawake waibuke na vipaji vyao,” alisema Balozi Mongella, aliyewahi kuhudumu kama Katibu Mkuu wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Wanawake.

Kuhusu hoja ya miaka 10 itoshe kuhudumu kwenye nafasi hiyo, alibainisha hiyo ni kazi inayopaswa kufanywa na waliopo sasa, baada ya uchambuzi wa kina kama uliofanyika wakati wa kuanzishwa kwa nafasi hizo.

Hoja hiyo inaungwa mkono na Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chadema, Jesca Kishoa aliyesema kama lengo la nafasi hizo ni kujenga uwezo wa wanawake kwenye uongozi, miaka 10 inatosha mwanamke kufuzu kuelewa mikiki ya siasa na uongozi.

“Hivyo anaweza kupambana kwenye nafasi ya jimbo na kuacha wengine pia wapate uzoefu huo,” alisema.

Jesca, anayehudumu nafasi hiyo kwa kipindi cha pili anasema uzoefu huo hautafutwi kwa zaidi ya kipindi hicho, vinginevyo kuwe na sababu ya msingi ambayo mwanamke huyo asipokuwepo bungeni kuna mkwamo utatokea.

“Kama lengo ni uwakilishi wa wanawake bungeni, basi ni wazi yeyote mwenye sifa anayo haki ya kuwa mwakilishi wa wengine.
Haipaswi awepo mtu mwenye hati miliki ya uwakilishi huo kwa muda mrefu sana,” alisema Jesca, aliyehudumu nafasi hiyo tangu mwaka 2020.
Alipoulizwa kuhusu hilo, aliyekuwa Mwenyekiti wa UWT taifa, Gaudensia Kabaka alisema ni vigumu kulifafanua sasa kwa kuwa bado ni pendekezo na halijafika mwisho.
“Kiitifaki sio vizuri kutoa maoni sasa hivi kwa kuwa ndiyo kwanza limependekezwa, bado hatujakaa vikao na halijafika kwetu, likiamriwa tutaanza mchakato wa kutekeleza, lakini kwa sasa siwezi kutoa maoni kwa kuwa bado ni pendekezo,” alisema.


Waliohudumu muda mrefu Subira Mgalu ni miongoni mwa wabunge wa viti maalumu waliohudumu kwa zaidi ya miaka 10, aliingia kwenye nafasi hiyo mwaka 2010 kupitia CCM, akiwakilisha kundi la wanawake.Mwaka 2015 aliukwaa tena wadhifa huo kupitia kundi la wanawake, pia aliibuka mwaka 2020 ambapo atahudumu hadi mwaka 2025 na hivyo kuwa mmoja wa wabunge wa viti maalumu waliohudumu vipindi vitatu hadi sasa.Lucy Mayenga ni mbunge mwingine aliyehudumu katika nafasi za viti maalumu kwa muda mrefu, tangu mwaka 2005 na sasa amefikisha vipindi vinne.

Janeth Massaburi pia ameota mizizi katika nafasi hiyo, mara ya kwanza aliitwaa mwaka 2005 baadaye 2015 aliteuliwa kuwa Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sasa kuanzia 2020 amewania na kushika tena wadhifa huo kupitia viti maalumu.
Chanzo Mwanchi 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments