Upigaji Kura Waendelea Handeni, Amani Yasisitizwa

Hali ya utulivu imeendelea katika vituo mbalimbali vya kupigia kura katika uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Vibaoni halmashauri ya mji Handeni mkoani Tanga huku ulinzi ukiimarishwa.

Wakizungumza baada ya kupiga kura leo Jumamosi Desemba 17, 2022, wagombea katika uchaguzi huo wamesema kuwa hali ni shwari.

Mgombea udiwani wa Chama Cha Wananchi (CUF), Hilary Kitangwa amesema anatarajia uhuru utakuwepo.

"Tunaomba wanaohusika kusimamia uchaguzi wahakikishe wanazuia viasharia vyote vya uvunjifu wa amani, sheria zizingatiwe katika vituo vya kupigia kura ili kulinda amani", amesema Kitwanga.

Marry Mntambo mgombea udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema amekuta hali ni tulivu katika vituo alivyopita huku akitoa rai kwa wananchi kulinda amani wakati wakisubiria matokeo ya uchaguzi huo.


"Nimeona wananchi wamejitokeza kwa wingi katika kupiga kura ni haki yao na wanatakiwa kufanya hivyo, jambo la msingi ni kulinda amani yetu baada ya uchaguzi huu" amesema Marry.

Katika uchagzi huo vyama viwili vya CCM na CUF ndivyo pekee vilivyosimamisha wagombea wa kiti cha udiwani baada ya aliyekuwepo Ramadhini Kuyugu kuachia nafasi hiyo kwa kupata kazi serikalini

Msimamizi wa uchaguzi Handeni mjini, Maryam Ukwaju amesema jumla ya wananchi waliojiandikisha katika daftari la mpiga kura katika eneo hilo la Vibaoni ni 4,186 ambapo vimeandaliwa vituo 12 vya kupigia kura.

"Hali ni nzuri kwenye vituo vyote nilivyopita kuanzia asubuhi hakuna malalamiko niliyopokea kutoka chama chochote mpaka sasa, mawakala wamefungua vituo mapema na upigaji kura unaendelea", amesema Ukwaju.

Mkazi wa Vibaoni Halima Nuru amesema hakuna usumbufu wowote ambao amekutana nao katika kupiga kura na kusema kuwa wapo tayari kupokea matokeo hayo baada ya upigaji kura.

Mwenyekiti wa ulinzi wa usalama na mkuu wa wilaya ya Handeni, Siriel Mchembe amesema usalama umeimarishwa vituo vyote, hivyo hakuna uvunjifu wa amani ambao utaruhusiwa kufanyika.

Niwapongeze vyama vya CCM na CUF kwa kutunza amani kuanzia kwenye kampeni mpaka sasa kwenye uchaguzi, hakuna uvunjifu wa amani umetokea hili ni jambo la msingi na ndio agizo la Rais Samia Suluhu Hassanj kuhakikisha uhuru wa demokrasia unakuwepo", amesema Mchembe.

Chanzo Mwananchi

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments