CHONGOLO AMBANA MKANDARASI ALIYEPEWA KAZI YA KUSAMBAZA UMEME VIJIJI 60 MVOMERO

Katibu  Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Daniel Chongolo amemtaka mkandarasi aliyepewa jukumu la kusambaza umeme kwenye vijiji 60 ndani ya wilaya ya Mvomero kuhakikisha anafanya hivyo kama mkataba unavyomtaka awe amesambaza umeme vijiji vyote ifikapo Februri 28 mwaka huu.

Chongolo ameyasema hay oleo Januari 29 mwaka huu wakati akizungumza na wananchi pamoja na wanachama wa CCM ambako pamoja na kupokea changamoto mbalimbali , amepokea malalamiko ya mkandarasi anayesambaza umeme kwenye wilaya hiyo kusuasuasa wakati wananchi hitaji lao kubwa ni umeme kwa ajili ya kuendelea na shughuli za kimaendeleo.

“Mpango wa  serikali kama ilivyopanga vijiji vyote lazima vipate umeme na Serikali  imeshatoa fedha na hizo fedha zipo tayari kwa hiyo tunachohakikisha huu mradi unatekelezwa. Huyu mkandarasi mkataba wake unamalizika Februari 28 , asilete hadithi atuambie mango wake mpaka Februari 28 atafanyaje kuhakikisha wananchi wanapata umeme.

“Maneno maneno hatutaki, umepewa fedha ya umma wananchi wanachotaka ni huduma ya umeme , na umeme sio starehe ni huduma muhimu.Tunataka umeme kwa hiyo nendeni mkajipange huyo bwana aweke umeme hawezi vunjeni mkataba, hatuwezi kuendelea na hawa watu, taratibu za kisheria zipo,”amesema Chongolo.

Ameongeza wananchi wanataka kuona fedha zinabadilisha maisha yao na hayo ndio malengo ya Serikali  na Serikali inayoongozwa na CCM haiwezi kukaa inasubiri miujiza.“Tunataka majibu kwa maandishi na kabla ya kuondoka tuone anasema atafanya kwa namna gani na tutapima kutoka kwenye karatasi kuja kwenye uhalisia.

“Wami Dakawa tumekuja sio kupiga hadithi tumekuja kutafuta matokeo na kutatua changamoto za wananchi hatupendi kuona mtu anapewa jukumu na fedha amepewa lakini inakuwa adhabu na machungu kwa wananchi kupata huduma, hayo sio malengo ya Serikali, si malengo ya  Rais na wala si  malengo ya Chama hicho ambacho kimepewa dhamana na watanzania,”amesema Chongolo.

Kuhusu kilimo hasa ya umwagiliaji Chongolo amewapongeza wananchi kwa kazi kubwa wanayofanya wana Mvomero hasa Dakawa na maeneo ambayo  kilimo ni sehemu ya maisha yao na kwamba Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali yake imeweka msukumo na kipaumbele namba moja ni kwenye kilimo cha umwagiliaji na hasa ambacho hakitegemei misimu ya mvua ambazo sasa hivi hazina uhakika

“Tayari mmesema awamu ya kwanza mmeshaletewa zaidi ya Sh.milioni 20 na awamu ya pili mmeomba milioni mbili bado hazijaja lakini umenieleza kuhusu mradi wa Ruhindo ambao Sh.milioni 900 zimewekwa pale una changamoto kidogo , mradi umekamilika huu mwaka wa tatu lakini haujazilinduliwa kuanza kazi.

“Nikuhakikishie Waziri mwenyewe wa kilimo na watalaam wake wanaohusika ndani ya siku tano hizi watakuja kushughulikia, Serikali haiwezi kuweka fedha inayokaribia Sh.bilioni moja halafu mwaka wa kwanza, wa pili ,wa tatu haileti matokeo tuliyokusudia.

“Tutakwenda kushikana mashati kuulizana vizuri nani anahusika na hili na kwanini umechelewa tunataka kuona matokeo kwenye kila ambalo tunalipanga, niwaambie hakuna mahali ambapo tutaacha jambo liende kienyeji,”amesema Chongolo.

Kuhusu changamoto ya daraja la Mzambarauni , Chongolo ametoa maelekezo kwa viongozi wa TARURA kuhakikisha wanakwenda kufanya tathimini na kuangalia jinsi gani watashughulikia daraja hilo ili kuondoa adha ambayo wananchi wanaipata hasa nyakati za mvua za masika.“Nendeni leo kagueni mjue linahitaji fedha kiasi gani ili kuweka daraja hata la chuma , tusubiri watoto wasombwe maji halafu ndio tukimbizane. Nendeni mkaangalie na mje mniambie.”

Aidha amesema yeye pamoja na wenzake wamefika Mvomero kwa ajili ya kuwatembelea wananchi wanawaongoza ili kuzungumza nao , wamemtembelea Katibu wa Shina namba 18 na ameeleza changamoto kadhaa ikiwemo  kutokamilika kwa  jengo la zahanati ambalo ujenzi wake umeanza tangu mwaka  2013.TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments