KOCHA MPYA SIMBA SC APEWA MIAKA MIWILI, AITAKA FAINALI YA MABINGWA AFRIKA

 SIKU chache baada ya kutangazwa kuiacha Vipers SC, Kocha Roberto Oliveira (Robertinho) rasmi ametangazwa kuwa Kocha Mkuu wa Simba SC kwa mkataba wa miaka miwili huku akitaja malengo ya kufika Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama malengo yake makubwa akiwa Klabuni hapo.

Akizungumza wakati wa utambulisho wake jijini Dar es Salaam, Kocha Robertinho amesema amekuja Simba SC kufanikisha malengo ya Klabu hiyo ikiwa sanjari na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (NBC PL) msimu wa 2022-2023 ambao unaendelea.

Kocha huyo anayeamini katika mipango mizuri ili kufanikisha malengo, amesema amefika Simba SC na malengo hayo ya kufika si tu Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika bali hata kufika Nusu Fainali na Fainali ya Michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

“Wakati nikiwa Vipers SC, mipango mizuri na malengo ni vitu ambavyo vilitufikisha kwenye malengo yetu ya kuwatupa nje ya Mashindano Klabu ya TP Mazembe ya DR Congo tena kwenye uwanja wao na sisi kutinga makundi,” amesema Robertinho 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Simba SC, Murtaza Mangungu amesema wamemchukua Kocha Robertinho wakiamini uzoefu wake katika kufundisha soka, hivyo wanaamini kufika malengo yao ya kufika mbali zaidi katika mashindano mbalimbali.

“Kocha Robertinho ana uzoefu mkubwa katika kufundisha soka, na sisi tumeamini uzoefu wake na tunaamini atatufikisha kwenye malengo yetu ambayo tumeyaweka kama Klabu,” amesema Mangungu.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments