MBOWE,PROFESA LIPUMBA, ZITTO WAFUNGUKA BAADA YA RAIS SAMIA KURUHUSU MIKUTANO YA HADHARA

 VIONGOZI wa vyama vya siasa nchini wamefurahishwa na uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wa kuruhusu Mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa nchini.


Rais Samia ametoa ruhusa ya kufanyika kwa Mikutano ya hadhara leo Januari 3,2023 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa 19 ambavyo vimesajiliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.

Wakizungumza baada ya uamuzi huo wa Rais Samia, viongozi wa vyama vya siasa wamesema wanampongeza Rais kwa kuruhusu Mikutano ya hadhara kwani wamekuwa wakiomba kwa muda mrefu lakini hatimaye sasa wameruhusiwa.

Akizungumza kuhusu uamuzi huo Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA) amesema wanapongeza hatua hiyo ambayo imefikiwa baada ya kufanyika kwa mikutano mbalimbali kati ya Serikali na vyama vya siasa.

"Tunampongeza Rais kwa kuruhusu mikutano ya hadhara, hadi kufikia hatua hii Kuna vikao vingi ambavyo vimefanyika na Rais ameamua kutoa maamuzi haya baada ya kushirikisha vyama vya siasa.Mikutano ya hadhara kikatiba ilikuwa ni haki yetu.

"Hata hivyo baada ya kuruhusiwa mikutano ya hadhara kazi iliyopo mbele yetu ni kuweka presha kwenye kubadlishwa kwa sheria hasa zinazohusu vyama vya siasa lakini tunakwenda kuweka presha kwenye kuhakikisha tunakuwa na Katiba ambayo itatenda haki kwa Watanzania wote,"amesema Mbowe .

Aidha amesema Tume huru ya Uchaguzi ni jambo ambalo nalo linahitaji sana na katika hilo Rais Samia amefungua milango kwa wadau wa vyama vya siasa na taasisi nyingine kushirikishwa katika kila hatua ya mazungumzo hadi mambo yawe sawa.

Pamoja na hayo Mbowe amesema katika kushughulikia masuala hayo na kupata maridhiano CHADEMA waliamua kusimamia katika sheria ambazo wamejwekea na hata pale walipokuwa hawakubaliani na baadhi ya mambo hawakuwa na nia ya kukwamisha bali walitaka kuona kila kitu kinakuwa sawa kwa maslahi ya Watanzania wote na hatimaye sasa wamefika pazuri.

Kwa upande wake CUF Profesa Ibrahim Lipumba, ametumia nafasi hiyo kuelezea kufurahishwa na uamuzi huo wa Rais Samia kuruhusu Mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa

"Chama cha Wananchi (CUF) tunampongeza Rais Samia kwa maamuzi haya ameanza mwaka 2023 vizuri, kuruhusu vyama vya siasa kufanya Mikutano ya hadhara ni jambo ambalo tumekuwa tunalihitaji kwa muda mrefu sana.Kuna changamoto nyingi ambazo tunahitaji kuzizungumza kwenye majukwaa ya siasa lakini hatukuweza ila huu ni Wakati wetu kwenda kuzungumza na Watanzania,"amesema Profesa Lipumba.

Ameongeza kitendo cha kuzuiliwa kufanya Mikutano ya hadhara ni kama walikuwa wamefungwa midomo,hivyo uamuzi wa Rais Samia ni wa kupongezwa kwani unafungua ukurasa mpya kwa wanasisa kuendelea na shughuli zao za kisiasa na kubwa zaidi Rais ameeleza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vitakuwa vikiimarisha ulinzi kwenye mikutano hiyo .

Kuhusu Katiba mpya Profesa Lipumba amesema ni hitaji muhimu la Watanzania na wamemsikiliza vizuri Rais Samia kwenye suala la Katiba ,hivyo wanaamini litapata muafaka mapema.

Wakati huo huo Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe, amesema kuwa amefarijika kwa hatua ambayo Rais Samia ameifikia na kwamba wamefika hapo baada ya kufanyika vikao mbalimbali vya wanasiasa pamoja na wadau lakini hatimaye wote sasa wako kwenye njia moja.

"Wakati tunaanza mazungumzo na Rais Samia kuhusu hali ya kisiasa nchini tulikuwa na mazungumzo na Serikali lakini tunakumbuka na CHADEMA nao walikuwa na walikuwa na mazungumzo yao na Rais,jambo la kufurahisha leo pamoja na kuanza kila mtu na njia yake lakini leo wote tuko kwenye njia moja.

"Pamoja na hili la Rais kuruhusu mikutano ya hadharani kwa vyama vya siasa naomba nimpongeze sana Rais ,hiki alichokifanya amethibitisha kufuata maneno yake wakati anakula kiapo , Rais anaishi kwenye maneno yake, tunampongeza sana,"amesema Zitto na kusisitiza RaisSamia amepita katika kiapo chake.

"Wakati anakula kiapo aliahidi kuweka mazingira mazuri ya uchaguzi, pia kutatua kero wanazokabiliana nazo wanasiasa ,alieleza atakavyotafuta maridhiano ya kisiasa nchini kwetu, hivyo lametekeleza ahadi yake kwa vitendo."
Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahimu Lipumba  akizungumza na Waandishi wa habari leo Ikulu jijini Dar es Salaam,mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kuzungumza na viongozi wa vyama vya siasa 19 ambavyo vimesajiliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA),Freeman Mbowe akizungumza na Waandishi wa habari leo Ikulu jijini Dar es Salaam,mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kuzungumza na viongozi wa vyama vya siasa 19 ambavyo vimesajiliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.
 

 Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments