Chongolo awataka vijana wakasome Veta kupata ujuzi wa kujiajiri

                  

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Daniel Chongolo, amewataka wazazi kutowaacha vijana kuendelea kukaa kijiweni na kuwa mabingwa wa kupiga soga, porojo na maneno na badala yake wawapeleke kwenye mafunzo ya ufundi kupata ujuzi utakaowawezesha kuwa na kazi za kufanya.

Chongolo ametoa wito huo leo Februari 27, 2023 wakati wa ziara yake katika Wilaya ya Manyoni na kupata nafasi ya kuzungumza na wananchi waliojitokeza kumpokea.

Amesema serikali inajenga vyuo vya Veta kila wilaya ili kuwapa vijana ujuzi utakaowawezesha kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana kwenye maeneo yao.


Katibu Mkuu Bw . Chongolo ameeleza kuwa  kumekuwa na changamoto nchini vijana wengi wanapomaliza vyuo wakiwa na shahada hawaamini kama wanaweza kufanya kitu kingine zaidi ya hiyo taaluma waliyonayo.

           

Aidha Katibu Mkuu akizungumzia mradi wa maji wa Kintiku Lusilile, amesema kabla hajaondoka  mkoani Singida cheti cha msamaha wa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambacho kimekwamisha kuanza kwa mradi huo awamu ya tatu kitakuwa kimepatikana.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amesema kama cheti cha msamaha wa kodi kingekuwa kimetolewa mkandarasi aliyepewa zabuni ya kujenga mradi huo angekuwa ameanza kazi.

Awali taarifa ya ujenzi wa mradi huo iliyotolewa na Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Manyoni,Shija Maduhu, alisema mradi huo utakapokamilika Disemba mwaka huu utahudumia vijiji 11 vyenye zaidi ya wananchi 55,000.

Katibu Mkuu Ndg. Chongolo yupo mkoani Singida kwa ziara ya kuimarisha Chama na kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM, ambapo ameongozana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Ndg. Sofia Mjema na Katibu wa NEC, Oganaizesheni Ndg. Issa Gavu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha CCM Mkoa wa Singida Bi Martha Mlata  amesema wanaendelea vizuri na utekelezaji wa miradi ya maendeleo licha ya changamoto chache wanazokabiliana nazo.


"Tunakukaribisha sana mkoani kwetu, wananchi wanajituma katika shughuli zao za kila siku za kilimo na ufugaji na sisi kama viongozi tunawahamasisha kufanya kazi kwa bidii," amesema Martha


Matukio Mbali Mbali Kwa Picha














Na Abdul Bandola Singida


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments