DC MANGOSONGO AWATAKA WATUMISHI WA HALMASHAURI YA WILAYA MBINGA KUWA WAADILIFU WA MAPATO YA SERIKALI

WATENDAJI wa vijiji na kata katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,wamelazimika kula kiapo cha uaminifu na uadilifu kwa ajili ya kwenda kukusanya na kusimamia mapato ya serikali.


Hatua hiyo inatokana na baadhi ya watumishi waliopewa jukumu ya kukusanya mapato kutoka kwenye vyanzo ikiwamo kituo(geti) la Kitai linalokusanya ushuru wa malori yanayobeba makaa ya mawe na mazao kujihusisha na wizi kwa kutopeleka sehemu ya fedha hizo benki kama inavyotakiwa.

Akizungumza baada ya kiapo hicho,Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo,amewaonya watendaji na watumishi wengine kujiepusha na matumizi ya fedha mbichi zinazokusanywa kutoka kwenye vyanzo vya mapato.

Badala yake, wahakikishe wanaisaidia serikali kukusanya mapato na maduhuli mengine na fedha zote zinazokusanywa zinapelekwe benki na sio vinginevyo.

Amewataka watumishi wa Halmashauri hiyo, kuhakikisha wanasimamia eneo la ukusanyaji wa mapato ili kuiwezesha Halmashauri kutekeleza miradi itakayoleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo.

Mangosongo ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki, wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri hiyo kwenye kikao kazi cha wadau wa makaa ya mawe kilichofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Kigonsera.

Amewasisitiza kufanya kazi kwa weledi,kutekeleza na kusimamia miradi ya maendeleo kwa uadilifu na uaminifu ili miradi hiyo ilingane na thamani halisi ya fedha zinazotolewa na serikali.

Katika hatua nyingine Mangosongo,amewakumbusha madiwani ambao ni wajumbe wa kamati ya fedha,kuwa na utaratibu wa kutembelea na kukagua miradi mara kwa mara ili kujiridhisha juu ya ufanisi wake badala ya kusubiri kupokea taarifa za wataalam.

Mangosongo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Mbinga,amemuagiza mweka hazina wa Halmashauri na watumishi wanaokusanya mapato kujipanga ili kutafuta namna bora ya kuongeza mapato.

Awali afisa wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa(Takukuru) wilaya ya Mbinga Blandina Hamis alisema,uchunguzi uliofanywa na taasisi hiyo umebaini kuwa,baadhi ya madereva wa malori yanayobeba makaa ya mawe hawalipi kiwango cha fedha kilichopangwa cha Sh.30,000 yanapopita geti la Kitai.

Alisema kuwa,kuna magari yanalipa fedha ndogo kati ya Sh.20,000,15,000 na 1,000 na kupewa listi ya kubeba mazao badala ya makaa ya mawe na mengine hayakatiwi listi,bali madereva wanalipa fedha kwa njia ya simu za wafanyakazi wa getini ,hivyo kuikosesha serikali mapato.

Mkuu wa Takukuru wilaya ya Mbinga Frederick Msae alisema,idadi ya malori yanayobeba makaa ya mawe na kupita katika geti la Kitai ni 300 hadi 450 na mapato yalikuwa Sh.milioni 2 hadi milioni 4 kwa siku.

Alisema, baada ya Takukuru kustukia mchezo mchafu unaofanywa na watumishi waliopewa dhamana ya kukusanya ushuru na kufanya uchunguzi wa kina sasa mapato yameongezeka hadi kufikia Sh.milioni 10.

Kwa upande wake Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo Samweli Marwa,amehaidi kuongeza udhibiti wa upotevu wa mapato katika geti la Kitai na maeneo mengine.

“Mheshimiwa Mkuu wa wilaya mimi na watu wangu tutajipanga upya kudhibiti upotevu wa mapato katika geti hili”alisema Marwa.


Mkuu wa Wilaya ya Mbinga ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama Azazi Mangosongo akizungumza katika moja ya vikao vya kazi na watumishi wa idara na taasisi mbalimbali za serikali wilayani humo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments