DC mpya Mbogwe aapishwa kuziba nafasi ya bosi CWT


 Hatimaye Sakina Mohamed ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita

Hatua hiyo imekuja baada ya Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Leah Ulaya aliyeteuliwaa kushika wadhifa huo Januari 25, kutofika kupishwa aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo.

Mbali na Ulaya, Katibu Mkuu wa CWT, Japheth Maganga naye hakwenda kuripoti wilayani Kyerwa Mkoa wa Kagera alikoteuliwa.  


Habari kutoka vyanzo vya kuaminika vya Mwananchi zimethibitisha kuwa Sakina ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa mtumishi wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) ameapishwa jana Februari 15, 2023 na anatarajiwa kuripoti kituo chake cha kazi kesho Februari 17, 2023.

Alipoulizwa kwa simu, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella hakuweza ama kuthibitisha au kukanusha kumwapisha Mkuu huyo mpya wa Wilaya ya Mbogwe, badala yake alisema; "Niko barabarani.”

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, Vicent Rubaga ameithibitishia Mwananchi kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa mkuu huyo mpya wa wilaya.

“Mbogwe tumefurahia kumpata Mkuu wa Wilaya kwa sababu nafasi hiyo imekaimiwa kwa muda mrefu na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe. Nimeambiwa ataripoti ofisini kesho na sisi tuko tayari tunamsubiri tushirikiana kuijenga Mbogwe yetu,” amesema Rubaga kwa njia ya simu leo Februari 16, 2023.

Wilaya ya Mbogwe imekosa Mkuu wa Wilaya kwa takribani mwaka mzima baada ya aliyekuwepo, Charles Kabeho kuondoka kimyakimya bila kujulikana alipo wala sababu za kutokuwepo ofisini.

Kabla ya kuteuliwa na kuapishwa kwa Sakina, nafasi hiyo imekuwa ikikaimiwa na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Said Nkumba.

Kuhusu hafla ya uapisho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbogwe, Vicent Rubaga amesema; “Aliapishwa jana (Februari 15, 2023); viongozi kadhaa tulihudhuria hafla hiyo wakiwemo wajumbe wa Kamati ya Ulinzi ya Wilaya na viongozi wa CCM (Chama Cha Mapinduzi).”


Maganga na Ulaya waliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa wakuu wa wilaya Januari 25, 2023, uteuzi ambao pia ulimhusisha Dinah Mathamani aliyeteuliwa na kuapishwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.Awali, Mathamani alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CWT kabla ya kuondolewa Desemba 16, mwaka jana.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments