DC MWANZIVA AITAKA ZIMAMOTO KUTOA ELIMU MASHULENI

Mkuu wa wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva ameitaka idara ya zima moto wilayani humo kupita katika shule mbalimbali na kutoa elimu juu ya athari za majanga ya moto na namna ya kupambana nayo kitu ambacho kitasaidia wanafunzi kujikinga wenyewe na kuzuia uharibifu wa mali mbalimbali za serikali.


Mkuu huyo ameyasema hayo alipotembelea shule ya sekondari Lugarawa ambayo siku kadhaa zilizopita iliunguliwa bweni la wavulana na hivi karibuni tena kutokea kwa jaribio la kuunguza bweni la wasichana ambapo moto wake uliweza kuunguza vitanda vitatu, shuka na blanketi.

Kutokana na matukio hayo mkuu huyo wa wilaya ameunda kamati ya uchunguzi wa matukio hayo itakayo shirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kubaini vyanzo vya moto pamoja na wahusika wake kitu ambacho kitasaidia kuondoa hofu kwa wanafunzi na kukomesha matukio hayo.

" Kutokea kwa matukio haya kunaweza kujenga hofu kwa watoto wetu waliopo hapa shuleni, hivyo naomba vyombo vya usalama na kamati iliyoundwa mkafanye uchunguzi huu kwa haraka na kwa weledi ili tuweze kupata ufumbuzi wake". Amesema Mwanziva.

Sanjari na hilo pia mkuu huyo amewapongeza wale wote waliojitoa kwa michango ya ukarabati wa bweni hilo la wavulana lililoungua awali ikiwemo ofisi yake, Halmashauri na Mbunge wa jimbo la Ludewa kwani ukarabati huo umekwisha anza kwa kasi na wanatarajia wanafunzi kuanza kulitumia hivi karibuni.

" Nawasihi vijana wangu mtulie na muendelee na masomo yenu kama kawaida, haya maswala yatafanyiwa kazi ipasavyo hivyo ninyi someni kwa bidii ili mkuze kiwango cha elimu katika wilaya yetu". Amesema Mwanziva.

Deogratius Massawe ni mkuu wa polisi wa wilaya ya Ludewa amewaomba wananchi na wanafunzi kuonyesha ushiririkiano wao katika kubaini wahalifu huku Diwani wa kata ya Lugarawa Erasto Mhagama akiahidi kuwa bega kwa bega na vyombo vya usalama katika kutoa taarifa juu ya kitakacho hisiwa ama kubainika.TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments