Dereva gari iliyobeba waombolezaji afariki ajalini, saba wajeruhiwa

Juma Magembe, dereva wa gari aina ya Toyota Coaster iliyokuwa imebeba waombolezaji kutoka Musoma mkoani Mara kwenda jijini Arusha amefariki dunia huku saba wakijeruhiwa.

Ajali hiyo imetokea jana Jumamosi, Februari 11, 2023, baada ya gari hiyo iliyokuwa na waombolezaji 29 kupindukia korongoni kwenye kona ya Logia Mjini Babati, mkoani Manyara.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, George Katabazi akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili, amesema ajali hiyo ilitokea jana asubuhi katika kijiji cha Singu, Kata ya Sigino barabara kuu ya Babati-Singida.

Kamanda Katabazi amesema chanzo cha ajali hiyo ni mfumo wa breki wa gari hilo kushindwa kufanya kazi kwenye eneo la kona kali na mteremko wa Logia kisha kutumbukia kwenye Korongo.

"Kwenye ajali hiyo amefariki dereva wa gari hilo Juma Majembe na mwili wake umehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti hospitali ya rufaa ya mkoa wa Manyara," amesema Katabazi.

Amesema ndani ya gari hilo, kulikuwa na abiria 29 na majeruhi wote wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara.

Mmoja kati ya mashuhuda wa ajali hiyo, Christopher Hotay amesema gari hilo lilipita eneo hilo kwa mwendo kasi na likamshinda dereva kwenye kona na mterelemko.

"Gari lilipinduka zaidi ya mara nne, tukasikia kishindo kikubwa kisha ukimya ukapita ndipo kelele za watu zikasikika tukawahi kuwasaidia majeruhi na kuwapa taarifa viongozi waliotoa taarifa polisi," amesema Hotay.

Katika kona hiyo ya Logia, mwaka 2022 watumishi watatu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mkoa wa Manyara walifariki dunia kwa ajali ya gari wakiwa kazini.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments