DIWANI TERRAT AITAKA TARURA KUJENGA BARABARA YA ENGONONGOY-LOSWAKI

 DIWANI wa Kata ya Terrat, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Jackson Ole Materi, amewataka wakala wa barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kuitengea bajeri barabara ya Engonongoy-Loswaki hadi Terrat kwani imeshikilia uchumi wa watu.


Ole Materi akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, amesema atashikilia shilingi kwenye bajeti ya TARURA endapo wasipoiweka kwenye bajeti ya mwaka huu wa 2023/2024.

Amesema kwa muda wa miaka sita amekuwa akiisemea barabara hiyo tangu mwaka 2016 kupitia kikao cha baraza hilo katika kuwasilisha taarifa za kila kata amekuwa akiwasilisha changamoto ya barabara hiyo hasa wakati wa mvua ila haijajengewa.

“Barabara hii ya kutoka Engonongoi kupitia Loswaki kwenda Terrat ni kubwa na inatumiwa mno ila nimeisemea kwa muda mrefu ili itengenezwe lakini hakuna utekelezaji,” amesema Diwani Ole Materi.

Amesema barabara hiyo inahudumia watu zaidi ya 4,000 na wanatumia barabara hiyo katika kusafirisha mazao yao hivyo anawataka TARURA wafikirie upya juu ya barabara hiyo.

Amesema Badala ya TARURA kuhudumia barabara hiyo kwa kutenga fedha ili itengenezwe, wenyewe wameanzisha barabara nyingine ili hali kipaumbele chao ilikuwa barabara hiyo.

“Sasa hivi TARURA hawapo chini ya Halmashauri ya Wilaya tena kama hapo awali ilivyokuwa hivyo  nadhani wanajiamulia kuweka bajeti ya kutengeneza barabara bila kutushirikisha sisi,” amesema Ole Materi.

Amesema yeye binafsi haungi mkono bajeti ya TARURA iliyopitishwa na ametoa mpendekezo yake ili yafanyiwe kazi kupitia barabara hiyo iliyopo kwenye kata ya Terrat.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Simanjiro, mhandisi Naftali Chaula, akiwasilisha mapendekezo ya mpango wa bajeti kwenye kikao cha baraza hilo la madiwani amesema barabara zitatekelezwa kwa kutumia fedha za mfuko wa jimbo, nyongeza ya tozo ya mafuta na fedha za miradi ya maendeleo.

Mhandisi Chaula amesema mapendekezo ya bajeti ya ukomo ni shilingi 897,430,00.00 bajeti isiyo ya ukomo ni shilingi 11,417,610.00, miradi ya maendeleo shilingi 1,500,000.00 mfuko wa jimbo shilingi 500,000,000.00 na nyongeza ya tozo ya mafuta shilingi 1,000,000,000.00.

Amesema baadhi ya barabara zilizotengewa fedha kwa ajili ya matengenezo ya kawaida ni Barabara ya Tairo-Nyiti ya kilomita 0.77 iliyotengewa shilingi 4,540,000.00 na barabara ya Masudi ya kilomita 3.84 iliyotengewa shilingi 22,660,000,00 za kata ya Mirerani.

Ametaja baadhi ya matengenezo ya barabara korofi ni Losinyai-Terrat yenye urefu wa kilomita 2, Ruvu Remit-Ngage kilomita 4, Lorbene-Olchoronyori-Kiruani kilomita 2, Msitu wa Tembo-Naisinyai kilomita 3, Nakweni-Komolo ya urefu wa kilomita 5, Langai-Lemkuna-Msitu wa Tembo kilomita 2 na Landai-Naberera.

“Barabara zilizotengewa bajeti ya matengenezo ya muda maalumu ni Nakweni-Komolo yenye urefu wa kilomita 2, Msitu wa Tembo- Naisinyai kilomita 1 na Lorbene-Olchoronyori-Kiruani kilomita 1,” amesema mhandisi Chaula.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments