Dk Mwigulu amshukia Mpina

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amemshukia Mbunge wa Kisesa (CCM) Luhaga Mpina akimtaka kuwa na uhakika juu ya taarifa anazotoa hasa zinazohusu masuala ya kiuchumi.

Akijibu hoja ya Mpina kwamba mfumuko wa bei umetokana na utekelezaji usio mzuri wa sera za fedha na mambo mbalimbali ikiwamo kufanya malipo nje ya bajeti, Dk Mwigulu amesema, “embu tujadili mambo mengine yanayohusu uganga wa kienyeji… kwenye uchumi hii ni taaluma yangu, mnajadilije vitu ambavyo viko wazi?”

Akichangia taarifa za Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira leo Februari 2, 2023 Dk Mwigulu amesema fedha zilizolipwa nje ya bajeti ni Sh86 bilioni baada ya kugundulika kuwa wanafunzi 29,000 waliokuwa wamedahiliwa kwenye elimu ya juu walikuwa nje kwa kukosa ada na kwamba fedha hizo zilitolewa baada ya Bunge kuazimia kuwa Serikali itafute fedha za kuwapa mikopo.


Dk Mwigulu amesema Serikali pia ilitoa Sh160 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 8,000 ili wanafunzi waliokuwa wakijiunga na shule waweze kuendelea na masomo akisisitiza kuwa kutoa fedha nje ya bajeti hakuwezi kusababisha mfumko wa bei huku akionyesha mshangao juu ya hoja kwamba kujenga madarasa kunasababisha mfumuko wa bei.

“Anapotokea mbunge na kusema tumetoa nje ya bajeti na kuishambulia Serikali kama vile imefanya uamuazi usio mzuri lazima kuwe na kasoro katika kufikiri kwake huwezi kuchukia fedha ambazo zinaenda kwenye ujenzi wa madarasa,” amesema.

Amesema angetamani kuona wabunge wakimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi huo wa kutoa fedha zilizowezesha wanafunzi wote kupata mikopo na kujenga madarasa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments