Dk Mwigulu Atoa Ahueni Ya Mfumuko Wa Bei


 Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema baada ya mwezi mmoja kuanzia sasa hali ya mfumuko wa bei za bidhaa haitakua kama ilivyo sasa.

Hiyo ni kutokana na hatua alizozitaja zilizochuliwa na Serikali ili kudhibiti mfumuko wa bei ikiwemo kuweka mikakati mbalimbali ya uzalishaji na kikodi.

Ameyasema hayo leo Jumatano, Februari 8, 2023, katika mjadala wa Mwananchi Twitter Sapce uliobebwa na mada isemayo Serikali imechukua hatua kukabiliana na mfumuko wa bei, nini maoni yako.

Pia, mjadala huo umeshirikisha watu mbalimbali wakiwemo wakulima, wanasiasa na viongozi wa serikali akiwemo Dk Mwigulu pamoja na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

Dk Mwigulu amesema ruzuku iliyotolewa kwenye mbolea na mafuta na mazao yatakayozalishwa katika maeneo yaliyotumia ruzuku yatakuwa kwa bei nafuu kuliko yale yanayozalishwa bila bei ya ruzuku.

"Haya (mazao) tunayotumia sasa hivi ni yale yaliyozalishwa mwaka jana, yaliyozalishwa kwa mbolea isiyokuwa na ruzuku, maana yake walitumia Sh120,000 hadi Sh140,000, mafuta hayakuwa na ruzuku, ndiyo yaliyokuwa juu na yalitumika katika usafirishaji na uzalishaji katika baadhi ya maeneo,” amesema

Amesema ukame uliokuwapo mwaka jana pia ulisababisha upungufu ambao kwa asili katika uchumi huwa ni chanzo cha mfumuko.

"Upungufu huu pia tunatarajia utakuwa umetibiwa kwa maana watu wamepata ruzuku hivyo watazalisha pakubwa zaidi kwa sababu gharama zitakuwa chini, mavuno yatakayofuata kama mvua zitakuwa zimenyesha."

Dk Mwigulu amesema,"sehemu zote zikipata mvua vizuri na mbolea kutumika vizuri tunatarajia suala la upungufu wa mavuno halitakuwepo, tutakuwa tumeongeza mavuno na kushusha gharama za uzalishaji kwa kutumia ruzuku zilizotolewa.”


Amesema hatua za muda mfupi zilizochukuliwa ni kutoa akiba ya mazao yaliyokuwepo huku akieleza suala hilo litaendelea.

Amesema hivi sasa pia Serikali inawaza kuanza kununua mchele kuwa sehemu ya akiba ya Taifa ili na wenyewe uwe unatolewa kwa ajili ya kwenda kupunguza bei ya bidhaa hizo zinapokiwa sokoni.


"Tunaamini baada ya mwezi mmoja kuanzia sasa, hali ya mfumuko wa bei za bidhaa haitakua kama ilivyo sasa,” amesema waziri huyo

"Waliohifadhi mazao wakiamini bei zitazidi kupanda niwasihi wayatoe sasa maana kwa hatua ambazo tunaendelea kuzichukua inawezekana bei ikawa chini kuliko wanavyotarajia," amesema Mwigulu.

Amesema Mawaziri wa fedha wa Afrika ya Mashariki wamejadili juu ya namna wanavyoweza kupunguza gharama za uingizaji ili kupata bidhaa zinazotoka maeneo mengine

Katika hilo, amesema wamengalia namna ambavyo mazao ya vyakula yalikuwa hayana kodi ya ongezeko la thamani (VAT) lakini yalikuwa na tozo ya uingizaji.

"Kwetu sisi bidhaa hizo hazijaja lakini kwa sababu sisi tulikuwa tunalisha ukanda mwingine uamuzi huo unatupa ahueni kwa sababu sisi tulikuwa tunalisha ukanda mkubwa," amesema Dk Mwigulu.

"Tunafanya haya yote kwa tahadhari sana kwa sababu masuala ya ratiba za mavuno yanaweza kuingiliana na akiba iliyopo.

Wakati waziri wa fedha akieleza hayo, awali, Dk Fanuel Ibrahim alihoji, Serikali imejibana kiasi gani kuhakikisha mfumuko wa bei unapungua.

"Hii ikiwa na maana imejibana vipi kwenye matumizi yake na kuweka fedha hizo kwenye bidhaa zinazotumiwa na wananchi. Kama ilivyofanyika kwenye mafuta ingeweza pia kufanyika kwenye bidhaa zitakazopunguza makali ya mfumuko wa bei kwa wananchi," amesema

"Nataka nijue Serikali imechukua jitihada gani za sasa hivi kumsaidia mwananchi," alihoji.

Naye Oscar Mkude ambaye ni mtaalamu wa uchumi amesema kwa kiasi kikubwa mfumuko wa bei umebebwa na sura ya kupanda kwa bei ya chakula.

Amesema kukosekana kwa misimu ya kilimo ni sababu ya kupanda bei hizi kutokana na mvua kuwa chache kumefanya mikoa inayozalisha mahindi na bidhaa za chakula zinazotumika kuwa chache na kufanya bei kupanda kila mwaka.

"Hata sasa, wakati mikoa mingine ikiandaa mashamba hali ya mvua bado inatishia kwa sababu haieleweki na haitabiriki itakuwaje, hii inaathiri sana katika uzalishaji,” amesema

Abdillah Nassor, amesema tija ya Serikali kuweka nguvu katika kilimo kwa kuweka ruzuku katika mbolea haitaonekana sasa bali baadaye.

"Faida tutaiona baada ya mavuno, bidhaa zitapungua bei, tofauti na ilivyo sasa, sasa hivi janga la mfumuko wa bei haijaikumba Tanzania peke yake, mfumuko wa bei umeikumba dunia nzima,” amesema na kuongeza:

"Mimi naishi Marekani, Marekani pia mfumuko wa bei umepanda kwa kasi, mwanzoni tulikuwa tukinunua petroli kwa dola 2 sasa tunanunua kwa dola 3 za kimarekani, mafuta ya kula yalikuwa kwa dola 1.5 sasa ni dola 3 za kimarekani hivyo mfumuko wa bei uko kila sehemu.”



TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments