HALMASHAURI NCHINI ZATAKIWA KUANDAA MAZINGIRA MAZURI YA UWEKEZAJI

 Maafisa Mipango kutoka halmashari mbalimbali nchini na Sekretarieti za Mikoa wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)Dk Grace Magembe akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais ,Angellah Kairuki kwenye hafla ya kufungua mafunzo ya siku kumi ya uandishi wa maandiko ya miradi ya kibiashara yanayofanyika kwenye manispaa ya Morogoro.

Maafisa Mipango kutoka Halmashauri mbalimbali nchini pamoja na sekretarieti za Mikoa wakifatilia mada mbalimbali kwenye mafunzo ya siku kumi ya uandishi wa maandiko ya miradi ya kibiashara.
.......

Maafisa Mipango wa Halmashauri pamoja na Sekretarieti za Mikoa wametakiwa kuandaa mazingira mazuri na wezeshi ya uwekezaji katika Mamlaka zao za Serikali za Mitaa nchini.

Rai hiyo imetolewa jana na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Miko na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dk Grace Magembe akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Angellah Kairuki kwenye hafla ya kufunga Mafunzo juu ya Uandishi wa Maandiko ya Miradi ya kibiashara ambayo yataziwezesha Halmashauri kufungua Makampuni.

Dk Magembe amewatata washiriki wa mafunzo hayo kutumia ujuzi walioupata ili waweze kuandaa mazingira mazuri na wezeshi yatakayo saidia wawekezaji kutoka sekta binafsi kuwekeza katika Halmashauri zao.

“Rais Dk Samia Suluhu Hassani ameifungua nchi kwa kujenga mazingira yanayowavutia wawekezaji kuja kuwekeza katika nchi yetu kutokana na ujuzi mlioupata nendeni mkaweke mazingira wezeshi katika Halmashauri zetu kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na nje ili waweze kuwekeza katika Halmashauri zenu kwa kufungua Makampuni," amesema Dk Magembe.

Aidha Dk Magembe amekipongeza Chuo cha Mipango pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kuandaa mafunzo yenye tija kwani yamejumuisha nadharia na vitendo kitu kilichowezesha washiriki kuibuka na maandiko ya kibiashara.

“Naomba niwapongeze na kuwashukuru Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kuandaa na kuendesha mafunzo haya yenye tija ” amesema Dk Magembe.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Prof Hozen Mayaya amesema mafunzo hayo elekezi yaliyofanyika kwa nadharia na vitendo yametoa jumla ya maandiko kumi na tatu ya kibiashara ambayo yataziwezesha Halmashauri kuyawasilisha kwenye taasisi za kifedha kwa ajili ya kupata mikopo ya kuanzisha Makampuni (SPV).

Naye Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Emmanuel Nnko akizungumza kwa njia ya mtandao amekishukuru Chuo cha Mipango kwa kufanya utafiti ambao ulibainisha changamoto ya ukosefu wa vyanzo vya uhakika vya mapato kwenye Halmashauri nchini na hivyo kuandaa mafunzo haya.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments