Yanga SC wamejibu madai ya Mdhamini wao Mkuu, Kampuni ya Sportpesa baada ya Klabu hiyo kushutumiwa kukiuka makubaliano ya mkataba baina yao na kuingia makubaliano na Kampuni nyingine katika udhamini wa Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, hatua ya makundi
Katika taarifa iliyotolewa na Klabu hiyo, imedai kuwa Klabu imesikitishwa na madai hayo kutoka kwa Mdhamini wao Mkuu, Sportpesa ambao wamedai kuwa Yanga kukiuka makubaliano ya mkataba baina yao. Yanga SC wamebainisha kuendelea kutambua vigezo na masharti yaliyoainishwa kwenye mkataba wao.
Yanga SC wamedai kuwa waliijulisha Sportpesa kuwa watatumia Mdhamini mwingine katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi kwa kuwa Sheria na Kanuni za Shirikisho hilo haziruhusu Mdhamini anayehusika na masuala ya ubashiri (Betting) katika hatua hiyo.
Hata hivyo, mnamo Januari 27, 2023, Sportpesa waliindikia barua Yanga SC kuwajulisha kutumia nembo mbadala ya Kampuni hiyo, nembo ya SpScore.com ambayo itakuwa mbadala wa Sportpesa. Yanga SC walijibu kuwa nembo hiyo (SpScore.com) ilikataliwa na CAF kutokana kuwa mshirika wa Sportpesa.
Yanga SC wamedai kuwa mkataba wao na Sportpesa hauzuii kutafuta Mdhamini mbadala, na huku wakiendelea kuwa na msimamo wao kuwa hawajavunja kipengele chochote cha mkataba wao na Kampuni ya Sportpesa.
Aidha, Januari 30, 2023 mnamo Saa 1:52, siku ya uzinduzi wa Mdhamini mwingine katika mashindano ya CAF Yanga SC wamesema kuwa walipokea barua pepe kutoka Sportpesa wakielekeza Klabu kutumia nembo ya ‘Visit Tanzania’ kwenye nafasi ya mbele ya Jezi hizo kwa ajili ya Michuano ya CAF, huku wakishinikiza Klabu kuhudhuria uzinduzi wake Januari 31, 2023 siku inayofuata katika Ofisi zake, Dar es Salaam.
Yanga SC wamedai kutafsiri kitendo hicho cha Mdhamini Mkuu wa Klabu hakina mantiki na kudai kuwa kitendo hicho kina nia ovu, huku wakidai kuwa nembo ya ‘Visit Tanzania’ sio mpango wa Sportpesa hivyo wasingeweza kutumia nembo hiyo bila maridhiano na Mmiliki wa nembo hiyo.
Wananchi wamedai kuwa hawajatafutwa na Taasisi yoyote kuhusiana na matumizi ya nembo ya ‘Visit Tanzania’ hivyo hawajakataa kutumia nembo hiyo kama ilivyoelekezwa na Sportpesa, pia wamedai kuwa hawana dhamira yoyote kukataa kutumia nembo hiyo ya ‘Visit Tanzania’, kwani tayari waliwahi kutumia nembo ‘Visit Zanzibar and Kilimanjaro’ kama sehemu ya kuhamisha Utalii nchini.
0 Comments