Sheikh Alhad ateuliwa kuongoza kamati ndogo ya elimu, afya na malezi CCM

Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Alhad ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Malezi kwenye Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam.

Kamati hiyo inajumuisha viongozi wa kiroho akiwemo Sheikh huyo wa Mkoa pamoja na mchungaji, huku ikielezwa kuwa ni katika kusimamia malezi ya kiimani kwenye malezi ya wananchi.

Sheikh huyo ni mwenyeki wa kamati hiyo kati ya kamati sita ndogo ndogo za Jumuiya hiyo zilizoundwa kuhakikisha zinasaidia kusukuma malengo ya kusimamia suala la malezi ya vijana mkoani hapo.


Akizungumza Dar es Salaam leo Jumamosi 25, 2023 wakati akitangaza kamati hizo pamoja na viongozi wake Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo mkoani, Khadija Ally Said amesema kamati hizo zitakuwa zinaisaidia kamati ya uendeshaji kutekeleza majukumu yake.

"Kamati hizi ndogo ndogo tumezigawa katika maeneo sita, ikiwemo kamati ya uchumi na maendeleo, hapa jumuiya itakuwa inabuni miradi kwa hiyo wanakamati watakuwa wanasimamia kuleta mageuzi tunayosudia," amesema.

Khadija amesema kamati  ya elimu afya na malezi ambayo ni ajenda yao kitaifa kutokana na uzito huo inaundwa na wataalamu na wamekuja na kaulimbiu ya ‘Malezi bora kwa mtoto faraja ijayo kwa mzazi na Taifa’.

"Kamati hii inaundwa na wataalamu ambao wataenda kutoa mafunzo elekezi kwa viongozi wa ngazi ya kata na mitaa. Kuna walimu waliopo mashuleni muda wote ambako wanasimamia malezi na maadili," amesema.

"Kusimamia malezi kwa vijana kuhakikisha wanazingatia malezi yanayoendana na utamaduni wa kitanzania,"amesema

Amesema kamati nyingine ni ya utamaduni michezo na mazingira na ikiwa na malengo ya kujenga mahusiano mazuri kati ya chama na wanachama wake.

"Tutakuwa na timu za wazazi katika Kata zetu na mashindano mbalimbali kwa ngazi za wilaya hadi mkoa na tunategemea tukifanya vizuri tutaenda hadi nje ya nchi," amesema.


Baada ya uteuzi huo, Sheikh huyo amesema ameupokea uteuzi huo na kwamba eneo alilopewa anauzoefu nalo na kwamba ni ndoto yake ya muda mrefu hivyo atakuwa anasimamia.

"Nitakuwa nashughulikia elimu afya na malezi ni jambo nzuri na katika fikra zangu nilikuwa na ndoto nalo kwa wakati wote kulifanya namshukuru uteuzi,"amesema.

Sheikh huyo ambaye ni Imamu Mkuu wa Msikiti wa Kichangani Magomeni amesema Watanzania wote ni mashahidi mmomonyoko wa maadili na malezi ni wimbo wa Taifa kwa sasa.

"Hakuna mji wala nyumba, mkoa au nchi iliyosalimika na malezi Kila siku tunaona vitu vipya vinakuja na kwa masikitiko juhudi zinachukuliwa lakini hazijafika panapokusudiwa," amesema.

Amesema anamuomba Mungu katika kamati aliyochaguliwa apewe nguvu ya kulisimamia kwa kina suala la malezi na ukizingatia nafasi yangu ni sheikh ni kuwakataza watu mambo mabaya na kufuata mazuri.


        

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments