Mbunge ataka Serikali irejeshe fedha walizotozwa watoto njiti


 Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Agnes Hokororo amehoji Serikali kama iko tayari kurejesha gharama walizolipa hospitali wanawake waliojifungua watoto njiti.

Agnes amehoji swali hilo leo Jumanne Februari 7, 2023 wakati akiuliza swali la nyongeza bungeni.

“Je Serikali iko tayari kurejesha fedha kwa wanawake wajawazito. Ninayo madai ya anayedaiwa Sh1.8 milioni katika Hospitali ya Muhimbili,”amesema.


Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel ametoa agizo kwa hospitali zote ukiwemo Mfuko wa Bima ya Afya kwamba suala la wanawake na watoto njiti wakati wote bima ya afya wakizaliwa kwenye hospitali zote watibiwe bure.

“Kuhusu ushahidi ulionao, naomba nikishakaa uje tulifuatilie tuone tunafanyaje, siwezi kukwambia kuwa itarudishwa lakini tutapata aliyefanya ili tuweze kumpa maelekezo,” amesema.

Katika swali la msingi, Agnes alihoji kwa nini huduma za afya kwa watoto njiti zinatozwa fedha ilhali Sera ya Afya ni huduma bure kwa watoto chini ya miaka mitano.

Akijibu swali hilo, Dk Mollel amesema utoaji wa huduma za afya kwa watoto chini ya miaka mitano wakiwepo watoto njiti kwa vituo vya Serikali na vile vya binafsi vilivyo na ubia na Serikali ni bure na ni takwa la Sera ya Afya.

Amesema ukamilishaji wa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote utamaliza utata huu kwa wananchi wanaotibiwa katika vituo binafsi vya huduma za Afya.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments