MCL Kuwapika Maofisa Habari Wa Serikali


 Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inaendesha mafunzo ya uandishi wa habari za infographics (takwimu katika picha) kwa wanachama wa Chama cha Maaofisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO).

Mafunzo hayo ya wiki tano, yatahusisha maofisa habari 25 kutoka taasisi tofauti za Serikali ambapo kila mmoja atakaa darasani kwa siku tano.

Infographics ni njia ya uwasilishaji taarifa kupitia uchambuzi wa takwimu katika picha ambayo humsaidia mwandishi kuelezea tukio kwa upana zaidi kwa kutumia namba badala ya maneno na katika nafasi ndogo.


Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa MCL, Bakari Machumu amesema kama kampuni haitakuwa mchoyo wa maarifa kidogo iliyonayo kwa sababu inaamini kupitia ushirikiano.

Amesema kadri dunia inavyobadilika na tabia za walaji zinabadilika. Sasa watu hawapendi kusoma vitu virefu na badala yake wanataka kupata taarifa kwa kusoma uchambuzi katika picha (visualization).

“Kama ni picha, mtu ataona picha ataelewa zaidi, kama ni katuni mtu ataelewa zaidi, kama ni taarifa zinazohusu tofauti ya siku moja na siku ya pili na zinahusu data nyingi, hizi infographics ndiyo mahali pake,” amesema Machumu.

“Kitu ambacho ungeandika kurasa kumi unakiweka katika summary (ufupisho) ya nusu kurasa na mtu anaelewa. Kwa sababu watu wengi wana ugonjwa wa kuogopa namba ukimuwekea kwenye picha za namna ile na michoro ambayo inarahisisha kutafsiri mambo inakuwa ni rahisi na inavutia.

Alitolea mfano namna watoto wanavyojifunza kwa haraka kupitia katuni huku akieleza kuwa uchambuzi wa data katika picha pia huweka urahisi kwa watu kukumbuka.

Sarah Kibonde ambaye ni Kaimu Mwenyekiti wa Tagco amesema anaamini njia hiyo mpya ya uwasilishaji taarifa kupitia uchambuzi wa takwimu itasaidia kupata wasomaji wengi na taarifa za Serikali zitawafikia wananchi kwa njia rahisi zaidi.


Lakini alitumia nafasi hiyo kuiomba Kampuni ya Mwananchi kuangalia namna ya kuwafikia maofisa habari wengi zaidi.

“Tagco ina wanachama zaidi ya 400, labda tuwaombe baada ya kumaliza watu wetu 25 tuangalie njia nyingine ambayo inaweza kutumika ili muweze kutusaidia zaidi,” amesema Kibonde.

Chanzo Mwananchi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments