Miili 16 Kuagwa Viwanja Vya Hospitali Rombo.

Miili 16 kati ya 20 ya watu waliofariki kwa ajali ya gari mkoani Tanga, imewasili jana Jumapili usiku wilayani Rombo na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Huruma ambapo leo Jumatatu itaagwa katika viwanja vya hospitali hiyo.

Miili hiyo ambayo ilitarajiwa kuwasili jana Jumapili saa nne usiku ikitokea mkoani Tanga na kupumzishwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya leo siku ya Jumatatu ambapo ndugu jamaa na marafiki wataaga wapendwa wao katika viwanja vya hospitali hiyo.

Ajali hiyo ilitokea Februari 4, katika eneo la Magira Gereza, Kata ya Magira Gereza, wilayani Korogwe, Barabara ya Segera - Buiko na kusababisha vifo vya watu 20 mpaka sasa.


Ndugu hao pamoja na majirani walikuwa  wakisindikiza mwili wa ndugu yao, Athanas Mrema (59) aliyefariki dunia Februari Mosi, kutokea jijini Dar es Salaam kuja mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya maziko ndipo walipokutana na ajali hiyo  mbaya.

Akizungumzia taratibu za kuaga miili hiyo kesho, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Kanali Hamis Maiga amesema mipango ya mazishi inaendelea vizuri na kwamba katika wilaya hiyo watapokea miili 16 ikitokea Tanga ambapo 14 ni ya familia moja.

Amesema miili hiyo itaanza kuagwa saa mbili asubuhi kesho Februari 6 ambapo Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ataongoza mazishi hayo kwa kushirikina na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo.

Amesema wilaya hiyo imeandaa magari 13 kwa ajili ya kubeba miili hiyo na yatakwenda kwa Eskoti ya Jeshi la polisi kufikisha miili kwenye familia ambazo zimepoteza wapendwa wao.

Akizingumza kwa niaba ya ukoo wa Mrema, Colman Mrema amesema tayari wameshaandaa maeneo ya  maziko  kwa ajili ya kuzika miili ya ndugu zao.

Baadhi ya miili itazikwa katika Kitongoji cha Kirungu Mokala, Kata ya Kelamfua Mokala, Keryo, Mengwe na Shimbi wilayani humo.


 Chazo Mwananchi 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments