Mkandarasi Kukabidhiwa Eneo Ujenzi Uwanja Wa Dodoma

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kuwa michoro kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Mpira wa Miguu jijini Dodoma umekamilika  na  mkandarasi atakabidhiwa  eneo Machi 2023.

Mhe. Mchengerwa amesema hayo Februari 02, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu hoja za wabunge, baada ya kuwasilishwa kwa Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Stanslaus Nyongo.

 Waziri Mchengerwa ameishukuru Wizara ya Fedha kwa kutoa fedha za kuanzia katika ujenzi wa viwanja hivyo ambapo amesema tayari zabuni kwa ajili ya ujenzi wa eneo changamani la Michezo jijini Dar es Salaam imeshatangazwa.


Ameongeza kuwa, Zabuni kwa ajili ya Ujenzi wa eneo la kuonesha Sanaa ( Arts Arena) imeshatangazwa, huku akisisitiza kuwa, ujenzi wa shule 56 za michezo unaendelea.

 Vilevile, Mhe.Mchengerwa ameeleza kuwa Wizara hiyo inaendelea kufanya mageuzi makubwa  ambapo imeanzisha Kampeni ya Sanaa mtaa kwa mtaa yenye lengo la kuibua vipaji kuanzia ngazi ya chini, huku akiwapongeza wasanii kwa kutumia vipaji vyao kuitangaza Tanzania.

 Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema Wizara imeendelea kufanya mapinduzi katika Sekta zake ikiwemo  mchakato wa kupata Vazi la Taifa, Mdundo wa Taifa pamoja na kutoa mikopo kwa Wasanii.

 Katika Hatua nyingine, Mhe. Mchengerwa ameeleza kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeitangaza Tanzania kuwa namba Tano katika nchi zenye ligi bora Afrika na namba 39 katika viwango vya kimataifa.

 Awali, akiwasilisha taarifa ya Kamati, Mwenyekiti Mhe. Nyongo ameeleza kuwa wizara imeendelea kutekeleza majukumu yake katika hali ya kuridhisha ambapo amesema Baraza la Sanaa la Taifa limefanikiwa kuanzisha mifumo ya kielekroniki katika kutekeleza majukumu yake, pamoja na kurudisha Tuzo za Muziki, huku akieleza kuwa Ofisi ya Hakimili nchini (COSOTA) imefanya maboresho katika maeneo mbalimbali kidigitali pamoja na kugawa Mirabaha kwa Wasanii ya takriban Milioni 300.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments