MRADI WA BOMBA LA MAFUTA UNAENDELEA KUTEKELEZWA-BYABATO

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amesema kuwa, utekelezaji wa mradi Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania (EACOP) unaendelea kutekelezwa na kwamba shughuli mbalimbali zinaendelea kufanyika nchini Tanzania na Uganda.


Naibu Waziri amesema hayo tarehe 10 Februari, 2023 wakati Wajumbe wapya wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiongozwa na Mwenyekiti, Mhe.Dunstan Kitandula walipopewa semina na Wizara ya Nishati kuhusu mradi wa Bomba la Mafuta (EACOP) , Nishati Safi ya Kupikia na ushiriki wa watanzania katika mradi wa EACOP. 

Semina hiyo ilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Byabato ametaja baadhi ya shughuli hizo kuwa ni pamoja na utwaaji wa ardhi ya mkuza wa bomba ambapo hadi tarehe 31 Januari 2023 jumla ya wananchi 8,781 wamesaini mikataba na asilimia 95.2 ya wananchi hao tayari wamelipwa fidia, na kwamba wananchi waliobaki wanaendelea kupatiwa elimu na kusainishwa mikataba ya fidia.

Aidha, amesema kuwa, ujenzi wa karakana ya kuhudumia vipande 86,000 vya mabomba yatakayotumika kwenye mradi huo, inayojengwa katika eneo la Sojo-Nzega umefikia asilimia 58.

Wajumbe hao pia walielezwa jitihada zinazofanywa na Serikali katika usambazaji wa nishati safi na salama ya kupikia vijijini ambapo moja ya juhudi hizo ni  usambazaji nishati ya gesi asilia kwa ajili ya kupikia katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani ambapo kazi hiyo inafanywa na TPDC kwa kushirikiana na REA.
Jitihada nyingine ni pamoja na kusambaza majiko banifu ambayo, hayatumii mkaa mwingi pamoja na kuni nyingi ambayo pia hayatoi moshi mwingi, pia, Serikali kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuongeza kasi ya upatikanaji nishati safi vijijini ikiwemo kujenga mitambo ya bayogesi katika taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 300.

Katika Semina hiyo Wajumbe wa Kamati pia walipata uelewa kuhusu EWURA inavyosimamia ushiriki wa watanzania katika mradi wa EACOP na jitihada zinazofanywa na Serikali ili kutatua changamoto mbalimbali zinazotokea kwa baadhi ya kampuni za kitanzania zinapopata changamoto ya utekelezaji wa kazi walizopata katika mradi huo.

Kamati hiyo ya Bunge pamoja na  kupongeza  Wizara ya Nishati kwa ubunifu wa mradi wa nishati safi ya kupikia, walitoa maoni mbalimbali yatakayoboresha utekelezaji wa mradi huo pamoja na miradi mingine ya nishati inayoendelea kutekelezwa nchini.Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Dunstan Kitandula  akizungumza wakati Wizara ya Nishati ilipotoa semina kuhusu  Mradi wa Bomba la Mafuta (EACOP), Nishati Safi ya Kupikia na ushiriki wa watanzania katika mradi wa EACOP   kwa Wajumbe wapya wa Kamati hiyo jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato na kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali.Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akizungumza wakati Wizara ya Nishati ilipotoa semina kuhusu  Mradi wa Bomba la Mafuta (EACOP), Nishati Safi ya Kupikia na ushiriki wa watanzania katika mradi wa EACOP   kwa Wajumbe wapya wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma.



TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments