Mvua ya mawe yaharibu ekari 102 za mazao


 Mvua ya mawe iliyoambatana na upepo imeharibu hekari 72 za mahindi na hekari 30 za mashamba ya parachichi pamoja na nyumba 14 kuezuliwa na nyingine kubomoka katika Kijiji cha Image kilichopo wilayani Njombe mkoani Njombe.

Hayo yamesemwa leo na katibu tawala wa Wilaya ya Njombe, Emmanuel George baada ya kufika kijijini hapo na kujionea hali halisi ilivyo ya uharibifu wa makazi na mazao ya wananchi uliotokana na kunyesha mvua kubwa. Amesema tukio hilo limetokea Februari 6, 2023 saa sita mchana na kusababisha madhara kwa wananchi baada ya mazao kuharibika pamoja na nyumba zao.


Amesema kutokana na mvua hiyo kuna nyumba zimebomoka na nyingine kuangukiwa na miti hali kama hiyo imeshajitokeza hapo mwaka jana na kuleta madhara makubwa.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ipo pamoja na wananchi hao ambapo baada ya tathmini kufanyika wataangalia namna ya kuwasaidia haraka iwezekanavyo wananchi hao.

"Serikali ya Mama Samia ipo pamoja nanyi tathmini imefanyika ili tuone namna ya kuwasaidia haraka iwezekanavyo" amesema George.

Wananchi waliokumbwa na majanga hayo wakiwemo Erika Imelo na Ester Zarambaya wamesema kutokana na tatizo hilo wanamashaka ya huenda wakakabiliwa na janga la njaa msimu huu.

"Mwaka huu tutakufa na njaa mimi heka tatu zote kwisha, hakukuwa na dalili ya mvua ilinyesha tu moja kwa moja, limvua la nguvu tukabidi tu tukimbie ndani, ilikuwa mvua yenye mawe makubwa ndani tulishindwa hata kupika, tulilala na njaa kwa sababu majiko yaliingia mawe yalikuwa makubwa, hatuelewi tufanye nini,"amesema Imelo.

Israel Mhada ambaye ni Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Lupembe, Edwin Swale,    alisema kuwa baada ya maafa hayo kutokea ofisi ya mbunge imetoa msaada ya bati 100.

"Baada ya kupata jambo hili mbunge tulivyomtaarifu kwa kuwa alikuwa ziara nje, alitamani kuwapo yeye mwenyewe kuja kuwapa pole. Kwa hiyo amenituma na kwamba leo tutakabidhi bati 100 ofisi ya kijiji ili wenyewe wafanye mgawanyo kwa watu waliopata majanga," amesema Mhada.


Naye Ofisa Kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Ibrahimu Fungo amewashauri wananchi hao kupanda mazao ya muda mfupi ili kukabiliana na majanga yaliyotokea.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments