Ndani ya Habari: Kwa nini wanaume wengi hawapimi VVU kirahisi?


 Ripoti ya utafiti inayoobainisha kuwa asilimia 35 ya wanaume wenye umri wa miaka 15 hadi 49 hawajawahi kupima kujua iwapo wana maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) ikilinganishwa na asilimia 20 ya wanawake.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya matokeo ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS) ya mwaka 2022.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 80 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wamewahi kupima kujua iwapo wana maambukizi ya VVU na walipokea majibu ya vipimo vyao ikilinganishwa na asilimia 65 ya wanaume wenye umri huo.


Hali hiyo inaelezwa na wadau kuwa wa masuala ya afya, kuwa wanawake wako katika nafasi ya kupima VVU kwa sababu katika maeneo mengi, hususani kipindi cha ujauzito, wanalazimika kujua hali zao.

Licha ya wanawake kuongoza katika kupima hali zao, imeelezwa kuwa chini ya asilimia moja ya wanawake wamewahi kupimwa na hawakupokea majibu yao.

Programu za upimaji VVU huchunguza watu ili watakaobainika kuishi na virusi waweze kuunganishwa na huduma za matumizi ya dawa za kurefusha maisha.

Uelewa wa hali ya maambukizi ya VVU pia husaidia watu wasio na virusi hivyo kupunguza hatari ya kupata maambukizi na kubaki salama.

Utafiti huo ilifanywa kwa kujumuisha makundi 629 ya kaya kwa hatua ya kwanza. Katika makundi hayo kaya 26 zilichaguliwa na kufanya jumla ya kaya zilizoshiriki kwenye utafiti kuwa 16,354 mwaka 2022.

Katika matokeo hayo, moja kati ya tatu ya kaya zilizochaguliwa zilikua za mijini na zilizobaki ni za vijijini.

Kila mkuu wa kaya alihitajika kujaza madodoso manne yaliyokuwa na maswali mambalimbali likiwemo la upimaji wa VVU.

Utafiti huo ulifanyika katika mikoa yote 31 ya Tanzania bara na visiwani.


Upimaji kwa ujumla

Licha ya matokeo hayo kwa wanawake, ripoti hiyo inaonyesha mwamko wa wasichana walio na kati ya umri wa miaka 15 hadi 19 kupima VVU bado ni mdogo kwani ni asilimia 37 pekee wamewahi kufanya hivyo na kuchukua majibu yao


Ikilinganishwa na waulana wa umri huo, takwimu zinaonyesha asilimia 19.4 wamewahi kupima ikimaanisha kuwa ambao hakujawahi kabisa kupima ni asilimia 81.6.

Si wao tu hali hiyo imeonekana pia kwa wanaume wenye umri wa kati ya miaka 20 hadi 24 ambapo asilimia 40.1 hawajawahi kupima VVU.

Kutokana na takwimu hizo, Dk Samwel Shitta alisema kisaikolojia mwanaume ni mtu wa kupuuzia mambo kuliko wanawake ambao mara zote huenda hospitalini kwa hiari yao kupima, waoga na mara zote wamekuwa wepesi kujisalimisha katika mambo mbalimbali kuliko wanaume.

“Hata katika mahusiano, wanawake wana wepesi sana wa kuulizia kupima kuliko wanaume, wakati mwingine wanaume ndiyo huchangia wanawake kutopima kwa kuwashawishi kuwa wako sawa,” alisema Dk Shita.

Anataja sababu nyingine ya wanawake kuongoza katika kupima UUV kuwa ni wakati wa ujauzito ambapo hulazimika kujua afya zao kwa ajili ya kumlinda mtoto.

Wakati takwimu zikionyesha hivyo, wanaume waliozungumza na mwananchi wamekuwa na mitazamo tofauti, baadhi wakisema kupima ni suala la kaiwaida kila mara na wengine wakisema wake zao wakiwa salama na wao wako salama.

“Mimi kila baada ya miezi mitatu napima kujua afya yangu, pia natumia njia zote kujilinda mimi na mwenzangu,” alisema Geofrey Phinigani mkazi wa Tabata.

Maoni yake ni tofauti na Joshua Kajuna ambaye anaeleza kuwa mkewe mara zote ndiye mwenye bidii ya kupima ili kujua hali yake na anaoona yuko salama basi naye huwa na uhakika kuwa yuko salama.


Hali ya maambukizo

Pamoja na matokeo ya utafiti huo, Tanzania ni moja ya nchi ambazo zinafanya vizuri katika kupunguza maambukizi mapya ya VVU.


Makadirio ya mwaka 2016 /2017 yalionyesha asilimia 61 tu ya watu walikuwa wanajua hali zao lakini hadi mwishoni mwa 2021 ni asilimia 89.7 walikuwa wanajua hali zao, kwa mujibu wa Tacaids.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaida, Dk Leonard Maboko alinukuliwa Novemba mwaka jana akisema Tanzania imetajwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ugonjwa wa Ukimwi (UNAIDS) kufanikiwa kupunguza maambukizi ya mapya ya VVU kutoka watu 110,000 hadi 54,000 kila mwaka

Alisema robo tatu ya maambukizi hayo mapya yanatokea kwa vijana.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments