Ndani ya Habari: Wabunge, Mawaziri Wazidi Kunyukana Kungeni

Wabunge na mawaziri waendeleza mnyukano bungeni kwa kila mmoja kuonyesha jinsi anavyomtetea mwananchi na Serikali katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kilimo, ubadhirifu na ugumu wa maisha.

Wabunge wamekuwa ‘wachungu’ dhidi ya mawaziri ambao wamekuwa wakisimama kidete kutetea Serikali kwa kujibu na kutoa ufafanuzi kwa hoja mbalimbali zinazoibuliwa.

Juzi, ilikuwa siku nyingine kwa mawaziri na wabunge kunyukana wakati wakijadili taarifa za utekelezaji shughuli za kamati za Bunge za Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Katika mjadala huo uliohitimishwa kwa taarifa hizo kupitishwa na kuwa maazimio ya Bunge, wabunge waliibua madudu ambayo mengi yanasabishwa na watendaji serikalini.

Mawaziri walionyooshewa vidole wao wenyewe au wizara zao ni, Hussein Bashe wa Kilimo, Dk Mwigulu Nchemba wa Fedha na Mipango, Angella Kairuki wa Tamisemi na George Simbachawene wa Sera, Bunge na Uratibu.

Mbunge wa Tandahimba (CCM), Katani Katani alisema kwa mwelekeo wa Serikali unavyokwenda haoni wanakwenda kufanikiwa hata kama Waziri Bashe anamaono makubwa kwenye kilimo.

“Nimesema hapa 2025 ukipata tani 700,000 za pamba. Katani nabaki Tandaimba na ubunge wangu nauacha huko huko nikalime korosho, hamna mipango ya namna hii,” alisema Katani aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia CUF kabla ya kwenda CCM

Alimweleza Bashe asipokuwa na utaratibu mzuri wa kuhakikisha fedha zinapelekwa kwenye sekta ya kilimo maneno yake yatakwenda kumtafuna.

Katani alisema kila mbunge anayesimama anaona kazi anayoifanya Rais Samia Suluhu Hassan na kuwataka wasaidizi wake kufanya tathimini ya kina wanapokwenda.

“Tunakwenda wapi. Mwigulu umetutukana wabunge sana na unapaswa utafakari utakapokaa. Hakuna anayeweza kujadili waganga wakienyeji hapa. Hakuna haya tunayoyajadili ni maisha ya Tanzania na tumletwa bungeni Watanzania hata iramba wanataka uwasaidie,” alisema.

Hata hivyo, Dk Mwigulu aliomba utaratibu na kusema kanuni za Bunge zinazuia kusema uongo sasa na kuwa mbunge anapojulisha Bunge kwamba yeye ametukana wabunge ni tuhuma kubwa sana.

“Bunge lako haliruhusu mimi nisingeweza kutukana wabunge na kiti kikiwepo pamoja aepuke kuwajumuisha,”alisema.

Akijibu hilo, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu alisema watakaa na sektarieti ya Bunge kutazama maneno ambayo mbunge amesema kisha watatoa majibu.


Hereni za ng’ombe

Mbunge wa Gairo (CCM), Ahamed Shabiby, alikosoa utaratibu wa uwekaji wa hereni kwa mifugo nchini akisema ufuatiliaji wake hauonyeshi mfugo uliowekewa alama unatoka wapi.

“Inawezekani kitu kama hiki huyu mama yetu Rais (Samia) hajui lakini nataka kusema wanakazi ya ziada upiganaji katika nchi hii uko waziwazi. Sisi wengine tunajua hata walio na zabuni hizo,” alisema Shabiby.

Alitaka Katavi walikofanyia majaribio ya kengele wawaamie ni ng’ombe wangapi wamekufa, waliochepuka na kuingia katika hifadhi.

Alisema wazungu wa bara la Ulaya wanatumia utaratibu huo lakini wanajua kila kitu kuhusiana na mifugo huku nchini za Kenya na Uganda hazitumii utaratibu huo.

“Mlianza na chapa, imeshindikana mmekuja kengele, kengele imekuja imeshindikana sasa hereni hereni ikishindikana mtataka wavae shanga za kiuno. Ikitoka hapo mtataka wavae vikuku vya miguu maana yake tunavisha ng’ombe,” alisema.

Mbunge wa Igalula (CCM), Venant Protas alitaka Serikali kutumia ushauri wa wabunge kutatua changamoto za wananchi.

Protas aliwataka mawaziri kuwasikiliza maana ndio kazi yao na kwamba wananchi walijipanga mstari kuwachagua wabunge kwa ajili ya kwenda kuwasemea kwa niaba yao.


Kuhusu kikotoo, mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu alisema bado kuna malalamiko ya kikotoo nchini.

“Tuliambiwa mambo mengi kuhusiana na kikotooo lakini ndani ya watumishi wa umma kinasumbua. Nimejaribu kukaa hata na Jeshi la Polisi tu wakielezea hawana muda wa kupumzika, hata kutafuta hela ya kuweka kibanda, unategemea ukilipwa mafao yako ndio uweke leo. Ukistaafu unalipwa kidogo (mafao ya mkupuo),”alisema.

Mbunge wa Tarime (CCM), Mwita Waitara alisema Serikali haiwezi kuwaambia Watanzania wachangie maendeleo wakati kuna fedha zinatumiwa vibaya na baadhi ya watendaji.

“Hatuwezi kuwaambia wananchi wachangie maendeleo wakati kapu limetoboka, tenga haliwezi kujaa, lina matundu kibao. Wabunge tumekutana katika Bunge hili kwa ajili ya Watanzania masikini. Wanatusikiliza lazima tuwe sauti ya wasiokuwa na sauti tufanye maazimio sahihi,” alisema.

Akichangia taarifa hizo kabla ya kupitishwa kuwa maazimio ya Bunge, Dk Mwigulu alisema malipo ya Serikali yanafanyika baada ya kazi kumalizika (kwa certificate), utaratibu uliopitishwa na Bunge na kuwa hawatoi fedha kulingana na bajeti iliyotengwa.

Kwa upande wake, Waziri Bashe alisema ni lazimia kumlinda mkulima bila kufanya uwekezaji katika miundombinu.

Waziri Kairuki alisema hatua mbalimbali zimechukuliwa na Serikali dhidi ya ubadhirifu.

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene alisema Serikali imechukua maazimio ya kamati zote tatu kwa mtazamo chanya na kuwa watayafanyia kazi.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments