Nyuki Wazusha Balaa Mazikoni


Nyuki wameibua tafrani katika makaburi ya Mburahati wakati wa maziko ya Erick Kwai (Emilian) na kusababisha watu kutimua mbio na wengine kujeruhiwa

Nyuki hao walisababisha kusimamisha shughuli za maziko kwa takribani dakika 20 huku majeruhi watatu wakipelekwa Kituo cha Afya Makurumla kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kwanza.

Erick ambaye kwa asili ni Mchaga alizikwa huku baadhi ya watu wakitafsiri kitendo hicho ni ishara ya mhusika kutoridhika kuzikwa makaburini hapo.


Erick aliyezaliwa Mei 1990, alifariki dunia Februari 4 mwaka huu baada ya kushambuliwa na wananchi kwa madai ya kumuua dada yake, Anna Thomas.

Siku moja baada ya tukio, mama mzazi wa Erick, Leornida Mosha alipozungumza na Mwananchi aligoma kufanya msiba wa mwanaye akidai hawezi kumzika muuaji huku akisema msiba anaoutambua ni wa Anna pekee.

Licha ya desturi ya watu kutoka Moshi kurudisha maiti katika mashamba ya ndugu pindi wanapofariki dunia lakini yeye alisema hawezi kurudisha muuaji.

“Hatuna mashamba ya kuzika wauaji, atazikwa Mburahati, hata sitahudhuria maziko yake, vitu vyake pia vilivyokuwa humu ndani tumevichoma hatuwezi kurithisha watu vitu vya muuaji, mimi namuomboleza Anna peke yake siyo huyo muuaji,” alisema.

Licha ya kugoma kuhudhuria maziko hayo, asubuhi ya jana baadhi ya majirani na Mwenyekiti wa Mtaa wa Kimamba, Magomeni Mwembechai, Ibrahim Awadhi walimsihi ili aweze kuhudhuria maziko hayo.

Mazungumzo hayo yaliyodumu kwa kipindi kirefu yalizaa matunda baada ya mama huyo kuungana na majirani wachache kuelekea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) mwili ulikokuwa umehifadhiwa kwa ajili ya ibada ya mazishi.

Licha ya yeye kugoma mwanaye asifanyiwe ibada, alisaliwa katika moja ya kanisa hospitalini hapo huku ibada ikongozwa na Mchungaji Imani Katana kutoka Kanisa la Moto Ulao Baptist lililoko Dege Kigamboni licha ya kuwa mama yake ni muumini wa Kanisa la Romani Katoliki.


Ibada hiyo kwa kiasi kikubwa ilijaa mahubiri yaliyowasihi watu kutohukumu kwa kuwa si jukumu lao na safari ya kuelekea makaburini ikaanza.

Tofauti na misiba mingine, msiba huu ulikuwa na wahudhuriaji wachache huku kukiwa hakuna aliyemwaga chozi kuanzia ndugu wa karibu na hata majirani.

Hata hivyo, shughuli ya maziko ilisitishwa ghafla baada ya nyuki kuvamia na kuanza kushambulia watu. “Inameni, laleni, kimbieni,” ni sauti zilizokuwa zikisikika kutoka kwa watu mbalimbali wakieleza namna ya kujilinda.

Baada ya zaidi ya dakika 20 kupita na namna ya kuwadhibiti nyuki hao kupatikana ikiwamo nguo chakavu kuchomwa na kuzalisha moto wa kuwafukuza, maziko yakaendelea.

Kuhusu maziko ya Anna, Mwenyekiti huyo wa Mtaa wa Kimamba alisema ipo haja ya kusitisha kwa muda ili kutoa nafasi kwa ndugu zake kuhudhuria ikiwa watapata taarifa.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments