PAC yataka CAG kukagua mifuko 52 ya Serikali


 Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa kina wa mifuko yote 52 ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kubainisha mapungufu yaliyopo katika mifuko hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka ameyasema hayo leo Jumanne Februari 7,2023 wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli za PAC kwa mwaka unaoanzia Februari mwaka 2022 hadi Januari mwaka 2023.

Amesema uchambuzi wa kamati hiyo umebaini kuwa kuna jumla ya mifuko 52 ya uwezeshaji wananchi kiuchumi na ambayo uendeshaji wake una mapungufu kutokana na uwepo wa mikopo chechefu na kunufaisha baadhi ya watu wasiostahiki.

Amesema usimamizi wenye dosari wa mifuko hiyo unasababisha matumizi mabaya ya fedha za umma na hivyo kuathiri malengo ya uanzishwaji wake ikiwa ni pamoja na uwepo wa mikopo chechefu.

Ametoa mfano katika kwa mifuko mitatu ya uwezeshaji wananchi kiuchumi mikopo chechefu ilikuwa takribani Sh50.04 bilioni.

Kaboyoka amesema ili kuimarisha usimamizi wa fedha za umma katika mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi inavyostahili Bunge linapaswa kuazimia masuala mbalimbali.

Ameyataja mambo wanayopaswa kuazimia ni Serikali ifanye tathmini ya kina na mapitio ya mifuko yote 52 ili kuangalia iwapo kuna sababu za msingi za kuendelea kuwa na mifuko hiyo yote kwa kuzingatia malengo ya uanzishwaji wa kila mfuko.

“Tathmini hii ikamilike kabla ya kukamilika kwa mwaka huu wa fedha na katika kipindi cha mpito, Serikali iimarishe udhibiti na usimamizi wa mifuko husika,” amesema Kaboyoka.

Aidha, kamati hiyo imetaka fedha zinazotolewa zitumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa na urejeshaji wa mikopo ufanyike kwa wakati.

“CAG afanye ukaguzi wa kina wa mifuko yote 52 ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ili kubainisha mapungufu yaliyopo katika mifuko hiyo,” amesema.

Amesema baada ya taarifa ya ukaguzi huo, Serikali ichukue hatua stahiki kwa kuzingatia matokeo ya ukaguzi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments