Polisi yataja sababu kuwatimua askari wake sita


 Jeshi la Polisi mkoani Arusha limewafukuza kazi askari wake sita katika kipindi cha miezi sita, kutokana na makosa mbalimbali ya utovu wa nidhamu yasiyoendana na maadili ya jeshi hilo.

Akiongea na vyombo vya habari ofisini kwake leo Febuari 20, 2023 bila kuwataja majina ya askari hao, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Justine Masejo amesema kuwa askari hao walifukuzwa kazi katika kipindi hicho baada ya uchunguzi wa kijeshi kukamilika kutokana na makosa yaliyokuwa yakiwakabili.

Amesema kuwa utaratibu wa kuchukuliana hatua za kinidhamu ndani ya Jeshi la Polisi ni jambo la kawaida hasa kwa askari wanapokiuka maadili ya jeshi hilo.

"Katika kipindi cha miezi sita tumewafukuza askari wetu sita, wakikabiliwa na makosa mbalimbali ya utovu wa nidhamu, kama mnavyojua askari wetu wanaoajiriwa wanatoka kwenye jamii, hivyo matukio ya utovu wa nidhamu lazima yawepo,"amesema Masejo.

Wakati huohuo, Kamanda Masejo amesema kuwa katika kipindi cha mwaka jana 2022, watu wapatao 241 walihukumiwa na kufungwa jela baada ya kufikishwa mahakamani kutokana na makosa ya ubakaji na ulawiti.

Amesema  kuwa,matukio ya ubakaji na ulawiti yamekuwa yakiongezeka ingawa jeshi hilo limekuwa likitoa elimu kwa jamii kupitia vipindi vya redio.

Katika tukio jingine Kamanda Masejo amesema kuwa Jeshi la Polisi limefanikiwa kumtia mbaroni mwanaume mmoja mwenye miaka 46 mkazi wa Sombetini jijini Arusha akituhumiwa kumlawiti mtoto wake wa kumzaa anayesoma darasa la kwanza.

Katika tukio jingine mahakama ya hakimu mkazi jijini Arusha imemkuta na hatia,Kelvin Wilfred (19) mkazi wa Muriet na kumhukumu kifungo cha Maisha jela kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wa darasa la nne.

Wakati huohuo Mahakama za Wilaya ya Karatu, Monduli na Arumeru zimewahukumu kifungo cha maisha watu wanne na wengine wanne wakihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kuwakuta na hatia katika makosa ya ubakaji na ulawiti.


Kamanda Masejo amewataja waliohukumiwa kifungo cha maisha kwa makosa ya ulawiti ni, Peter Leonard (27)mkazi wa Lashaine, Monduli, Paulo Hilonga (60) mkazi wa Karatu, John Sanare mkazi wa Arumeru na Elias Ndosikoi mkazi wa Arumeru.

Amesema wengine waliohukumiwa kifungo cha miaka 30 kwa makosa ya ubakaji ni James Elirehema, Elias Robert (27), Japhet Mungure wote wakati wa Arumeru pamoja na Theophili Salaho (32) mkazi wa Karatu.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments