RAIS SAMIA ATOA BIL 5.9 KUBORESHA AFYA YA MIFUGO

Katika kuboresha huduma za mifugo na kuiepusha dhidi ya magonjwa, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa Shilingi Bilioni 5.9 kwa ajili ya ujenzi wa majosho 257 katika halmashauri 80, ambapo majosho 88 yamekamilika.


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amebainisha hayo (19.02.2023) katika Kijiji cha Narakauo kilichopo Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wakati akihitimisha ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo kukagua miradi ya ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya mifugo, huku akibainisha majosho ambayo yapo katika hatua mbalimbali za ujenzi ni 169.

Akizungumza na jamii ya wafugaji Mhe. Ulega amesema katika kuhakikisha lengo na dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuokoa afya ya mifugo ya wafugaji katika mwaka wa fedha 2022/23, vifo vya mifugo vinavyotokana na maradhi ya kupe na ndorobo vimepungua kutoka asilimia 72 hadi 56.

Ameongeza kuwa tayari majosho matano yamejengwa katika Wilaya ya Simanjiro mwaka huu wa fedha, majosho mawili mwaka uliopita na majosho saba yatajengwa mwaka ujao wa fedha.

Aidha, amesema licha ya ujenzi wa majosho serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa dawa ya ruzuku kwa ajili ya kuweka kwenye majosho lita 52,560 kote nchini zenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.3, huku takriban lita 400 zikipelekwa katika Wilaya ya Simanjiro kwa ajili kuzitawanya katika majosho yaliyopo kwenye wilaya hiyo.

Kuhusu ombi la wananchi la mitego ya kukamatia mbung’o ambao wamekuwa wakisumbua kwenye maeneo yao Naibu Waziri Ulega amesema serikali imechukua ombi lao na litafanyiwa kazi ili kutafuta namna bora ya kutokomeza mbung’o ambao wamekuwa wakisumbua wananchi na mifugo.

Naye Diwani wa Kata ya Loibosiret Bw. Ezekiel Lesanga licha ya kuwa tayari kata yake ina majosho amepongeza juhudi za serikali na kuomba kuongezewa majosho mengine mawili ili kusogeza huduma karibu zaidi kwa wananchi wa Kata ya Loibosiret ambao mifugo yao iko katika maeneo mbalimbali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Bw. Baraka Kanunga ametoa pongezi kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa wanapata maji kupitia bwawa lililojengwa na serikali katika Kijiji cha Narakauo kwa gharama ya Shilingi Milioni 413 na kukabidhiwa Mwezi Mei Mwaka 2022, kwa ajili ya kunyweshea mifugo na matumizi mengine ya kibinadamu.

Bw. Kanunga amewataka wakazi wa Kijiji cha Narakauo kutoharibu bwawa na kwamba wanaweka mikakati ya kulizungushia uzio na kuweka miundombinu ya kupata maji hayo nje ya bwawa hilo.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) ametembelea na kujionea mradi wa ujenzi wa bwawa la Lelarumo katika Wilaya ya Simanjiro, litakalojengwa na serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 kwa gharama ya Shilingi Milioni 364.

Muonekano wa bwawa la maji kwa ajili ya mifugo na matumizi mengine ya kibinadamu ambapo serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejenga kwa Shilingi Milioni 413 na kulikabidhi katika kijiji hicho Mwezi Mei Mwaka 2022, ambapo wananchi wamemshukuru Rais Samia kwa kuwaondolea adha ya maji kwa ajili ya mifugo yao. (19.02.2023)

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments