Rais Samia awapa Rita maagizo matatu


Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), imeagizwa ihakikishe watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano na wale waliopo katika taasisi za elimu wasajiliwe na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa ifikapo mwaka 2025.


 Taasisi hiyo imetakiwa ihakikishe inaweka mkakati wa kuwasajili watu wazima na kuwapa vyeti vya kuzaliwa ifikapo mwaka 2030.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Februari 8, 2023 imesema maelekezo hayo yalitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, lakini yalisomwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro wakati akizindua Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Rita jijini Dodoma.


Pia, Dk Ndumbaro amesema lazima usajili ufungamanishwe na taasisi za elimu ili wakati wa kujiunga na elimu ya awali, msingi, sekondari na elimu ya juu wale wote wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa wapate fursa kupitia kambi maalumu ya usajili zitakazoanzishwa katika maeneo yao.


Kwa mujibu wa Dk Ndumbaro, usajili wa matukio muhimu ya binadamu ni nyenzo muhimu ya kuipatia Serekali takwimu muhimu katika kupanga mipango ya maendeleo na usalama wa nchi hivyo ni muhimu mchakato huo ukafanyika sasa.

 “Kuanzia sasa usajili ufanyike kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali zote za Serikali na watu binafsi, kwenye taasisi za elimu, kuanzia shule za awali, msingi, sekondari na vyuo mbalimbali lengo likiwa kuwafikia wananchi wengi zaidi,”amesema  Ndumbaro.

Dk Ndumbaro ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya sheria, ameitaka bodi hiyo kuishauri wizara kuhusu mambo ya kisera na utekelezaji wa majukumu ya Rita ili kuisaidia Serikali katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.


“Fanyeni kazi kwa uadilifu na uweledi wa hali ya juu kwa maslahi mapana ya nchi yetu kulingana na sheria na kanuni husika ili Rita ikidhi matarajio ya wadau na kuleta tija katika utekelezaji wa majukumu yake,”amesema Dk Ndumbaro.

Waziri huyo, amesema hivi sasa kuna migogoro mingi katika bodi za wadhamini wa taasisi za kidini, vyama vya michezo na vyama vya siasa kwa baadhi ya wadhamini kugombea mali na wengine kuzuia hati za umiliki wa ardhi na majengo ya umma kwa maslahi yao binafsi.

“Kupitia bodi hii wizara itapokea ushauri na mapendekezo ya namna bora ya kuweka mifumo au sheria itakayoelekeza majukumu, wajibu na mipaka ya wadhamini ndani ya taasisi husika ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza hivi sasa,”amesema.


Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dk Amina Msengwa amesema watahakikisha wanafanya kazi kwa pamoja na wizara na menejimenti ya Rita kwa kusimamia malengo na mikakati mbalimbali kwa kuwekeza zaidi katika mifumo ya kisasa ya utoaji wa huduma bora Kidigitali.

Wajumbe wengine wanaounda bodi hiyo ni Angela Anatory ambaye ni katibu, Profesa Abel Kinyondo, Erick Kitali, Theresia Mganga, CPA Peter Mwambuja na Wakili Lucy Dinganyeki.

 Chanzo Mwananch

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments