Serengeti sasa kujenga lami hifadhini

Uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti upo katika mchakato wa kujenga barabara za hifadhi hiyo kwa kiwango cha lami ili kupunguza gharama zinazotumika kuzikarabati mara kwa mara.

Katika kipindi cha miezi sita iliyopita hifadhi hiyo imetumia zaidi ya Sh13.4 bilioni kukarabati barabara zake na wakati mwingine walilazimika kukarabati barabara moja zaidi ya mara tatu kwa mwezi kutokana na wingi wa magari.

Akitoa taarifa ya hifadhi hiyo kwa wajumbe wa kikao cha bodi ya barabara mkoani Mara, Ofisa Mhifadhi Mkuu, Davis Mushi, alisema tayari wameanza mchakato wa kuomba kibali kwa ajili ya ujenzi huo kutoka kwa mashirika ya kimataifa ikiwemo Unesco ili waruhusiwe kujenga barabara kwa kiwango cha lami.


“Serengeti ni urithi wa dunia hatuna mamlaka ya kufanya uamuzi wa kujenga lami tushirikishe na kutafuta ushauri wa mashirika ya kimataifa la sivyo watatutenga,”alisema

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee, alisema umefika muda sasa barabara za hifadhi hiyo zijengwe kwa kiwango cha lami ili kupunguza matumizi.

Alisema endapo hifadhi hiyo haitatafuta suluhisho la kudumu kuhusu barabara hizo upo uwezekano wa fedha zote zinazopatikana zikatumika kukarabati barabara pekee.

“Tumeambiwa baada ya Royal Tour watalii wameanza kuongezeka sasa tusipoangalia hatutabaki na kitu chochote kwani fedha zote zitakuwa zinatumika kukarabati barabara na kama moja inakarabatiwa hadi mara sita kwa mwezi lazima kutafuta njia ya kudumu angalau zikae hata kwa miaka minne ili fedha zitumike kwa shughuli nyingine za maendeleo ya nchi yetu,” alisema

Awali, akifungua kikao hicho, Mzee aliwataka viongozi wa Serikali kusimamia miradi yote ili itekelezwe kwa wakati na kuzingatia thamani ya fedha akidai miradi mingi mkoani humo haitekelezwi kwa wakati kwa sababu baadhi ya viongozi hawatimizi wajibu wao.


Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania ( Tanroads) Mkoa wa Mara, Vedastus Maribe alisema changamoto inayowakabili katika utekelezaji wa majukumu ni pamoja na ucheleweshaji wa malipo kwa makandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments