Serikali Kuwafikishia Umeme Wachimbaji Wadogo Chunya


 Serikali imetoa zaidi ya Sh2.7 bilioni kwa ajili ya kusambaza nishati ya umeme kwenye maeneo ya migodi ya wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu wilayani Chunya.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera leo Jumatatu, Februari 6, 2023 wakati akitoa taarifa ya kuanza maonyesho ya teknolojia ya madini na fursa za uwekezaji yanayotarajia kufanyika wilayani Chunya Februari 21 hadi 25 mwaka.

Homera amesema katika maonyesho yenye lengo la kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta hiyo yatafunguliwa na Waziri wa Madini, Dotto Biteko.


“Kwa Wilaya ya Chunya pekee wastani wa kilo 350 mpaka 380 za madini zinauzwa katika soko la madini na kuchangia Serikali mapato ya zaidi ya Sh2 bilioni kwa mwezi,” amesema.

Amesema kutokana na mchango huo Rais Samia Suluhu Hassan ametoa eneo lenye ukubwa wa ekari 2,000 ambazo wanaendelea shughuli za uchimbaji, ikiwepo ujenzi wa duka kubwa la vifaa vya ulipuzi  kwenye miamba sambamba na kituo cha jiolojia cha kufanya utafiti kwenye miamba.

Amesema kupitia maonyesho hayo, Serikali imetoa fursa kwa wawekezaji wakubwa na wa kati kushiriki kikamilifu ili kuona teknolojia za uwekezaji katika sekta ya madini kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali.

“Wadau mbalimbali watashiriki zikiwemo taasisi za fedha ambazo tumezitaka kutoa mikopo kwa wachimbaji hususan ya upatikanaji wa vifaa ili kuboresha teknolojia rahisi katika shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu wilayani humo,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya One voice, Thomas Vungwa amesema kuwa maonyesho hayo yatakuwa ya tofauti yenye lengo la kukuza na kuboresha shughuli za wachimbaji wadogo wa madini wilayani chunya.

“Tumekuja na ubunifu mkubwa wa  tofauti kabisa  katika maonyesho  yakisekta   kwa  kutangaza fursa za madini katika wilaya ya chunya kwa kuwakutanisha wadau mbalimbali ili kufikia malengo  kukuza sekta hiyo kama mikoa mingine,” amesema.


Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Mbunge wa Jimbo la Lupa, Masache Kasaka amesema kuwa maonyesho hayo yatakuwa ni fursa kwa wachimbaji wadogo wilayani humo kutanua wigo wa kutumia teknolojia rahisi ya uchimbaji.

 “Kwanza niishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kipekee kufikisha nishati ya umeme kwenye maeneo ya migodi ya wachimbaji wadogo, kwani kulikuwepo na changamoto ya upatikanaji wa nishati,” amesema Masache.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments