Serikali Yatoa Mwongozo Mahindi Ya Bei Nafuu Na Ugawaji Bure


 Serikali imetoa mwongozo kwa halmashauri ambazo zinakabiliwa na njaa na kuhitaji chakula cha bei nafuu au msaada kwa wananchi wake.

Utaratibu huo ni Mkurugenzi wa Halmashauri husika kuandika barua kwa Waziri Mkuu kupitia Wizara ya Sera, Bunge na Uratibu ambao ndiyo wenye jukumu la kutoa kibali kwa wataalamu kujiridhisha kama kweli kuna uhitaji wa chakula.

Mwongozo huo umetolewa bungeni leo Februari 3, 2023 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Bunge, George Simbachawene wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Ferister Njawu.

Mbunge huyo alihoji ni mkakati gani ambao Serikali inachukua katika kuwasaidia Watanzania katika maeneo mengi ambako wanakabiliwa na baa la njaa kwa sasa.

Kauli ya Simbachawene ni kama imefunga milango kwa wabunge na viongozi wa halmashauri ambao wamekuwa wakielekeza maombi ya mahitaji ya chakula kwa Wizara ya Kilimo.

“Ofisi ya Waziri Mkuu ikishapokea taarifa hiyo, itaagiza wataalamu kutoka wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ambao watakwenda kujiridhisha kama eneo hilo linahitaji chakula cha bei ndogo atatafutwa wakala na kama kunahitajika chakula cha bure taarifa itaeleza,” alisema Simbachawene.

Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mzava (CCM) alihoji Serikali ina mpango gani wa kusaidia upatikanaji wa chakula cha bei nafuu kwa wananchi walioathirika na ukame wa chakula.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde alisema Serikali kupitia NFRA imeendelea kutoa chakula na kukiuza chini ya bei ya soko.

Mavunde amesema hadi Januari 31, 2023 kiasi cha tani 24,975.152 zimepelekwa na kuuzwa katika halmashauri 60 nchini katika vituo vya mauzo 116.


“Katika Halmashauri ya Korogwe, kituo cha mauzo kimefunguliwa eneo la Masewa tangu Januari 27 mwaka huu na tani 32 zimepelekwa na tayari tani 10 zimeshanunuliwa,” amesema Mavunde.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri, eneo lingine lililopelekwa chakula cha bei nafuu ni Wilaya ya Iringa Vijijini ambako linapatikana Jimbo la Karenga alikosema mahindi yataanza kupelekwa kesho Februari 4, 2023.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments