SERIKALI YATOA UFAFANUZI KUHUSU WATAHINIWA WALIOFUTIWA MATOKEO YA MITIHANI KIDATO CHA NNE 2022.

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa ufafanuzi kuhusu watahiniwa waliofutiwa matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2022.

Akitoa ufafanuzi huo Jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari, Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema kati ya watahiniwa 560,335 waliofanya mtihani, 337 ndio waliofutiwa matokeo na wengine 20 matokeo yao yamezuiliwa yakisubiri uchunguzi kukamilika.

Waziri Mkenda amesema kuwa kati ya waliofutiwa matokeo wanne waliandika lugha isiyo na staha, 51 walikutwa na maandishi yasiyoruhusiwa ndani ya chumba cha mtihani, 10 walikamatwa na simu na smart watch, 9 walifanyiwa mtihani na watu wengine na 27 walikamatwa wakisaidiana katika chumba cha mtihani.

"Wengine sita kutoka kituo cha Mnemonic, Zanzibar waligundulika kutumia jukwaa la WhatsApp kupata majibu kutokana na yule mmoja aliekutwa na simu, 206 walikuwa na mfanano wa majibu usio wa kawaida ukihusisha kituo cha mtihani cha Thaqaafa, Mwanza na Twibhoki Mara , huku 24 wa kituo cha Cornellius ambacho pia kilikuwa na watahiniwa kutoka shule ya Andrew Father Memorial waligundulika kupewa majibu kabla ya kuingia chumba cha mtihani," amefafanua Prof. Mkenda.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa Serikali inafanya jitihada kumaliza kabisa tatizo la udanganyifu na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watumishi wa umma wote watakaobainika kuhusika na udanganyifu huo.

"Gharama za kuendesha mitihani ni kubwa sana; kufanya udanganyifu ni sawa na uhujumu uchumi hivyo watumishi wote watakaobainika kuhusika  watafukuzwa kazi na kushtakiwa," amesema Prof. Adolf Mkenda.

Katika hatua nyingine Waziri Mkenda amesema Serikali imeanza mchakato wa kubadilisha sheria ya kudhibiti wizi wa mitihani ili kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa kwa wanaofanya udanganyifu na kuongeza kuwa ili kuhakikisha ubora wa elimu unalindwa ni muhimu kuhakikisha tunaepuka udanganyifu.

"Kubwa zaidi ni kuwa na maadili na uadilifu. Mtoto mdogo akifundishwa kuwa ili afanikiwe ni lazima aibe, hiyo ni kulibomoa taifa. Lazima tuwe makini na tusimame kidete kuhakikisha tunasimamia maadili katika elimu yetu," ameongeza Waziri Mkenda.

Aidha Prof. Mkenda amewataka wazazi na walezi ambao wanahitaji taarifa zaidi wawasiliane na  Baraza la Mitihani au hata Wizara ya Elimu ili kupata ufafanuzi.

Mkenda ameongeza kuwa uchunguzi unaendelea kupitia jeshi la Polisi katika  maeneo mbalimbali huku akieleza baadhi ya watuhumiwa wako chini ya ulinzi.Waziri wa Elimu  Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dodoma. Kulia ni Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Omari Kipanga.Waziri wa Elimu  Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda (Katikati) kulia ni Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga na kishoto ni Katibu wa Elimu Sayansi na Teknolojia Francis Michael wakiwa katika mkutano na wanahabari  leo jijini Dodoma. 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments