Serikali Yatoa Ufafanuzi Utangazaji wa Shule Bora


 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amepigilia msumari uamuzi wa Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) wa kutotangaza shule na wanafunzi bora huku akieleza utaratibu wa zamani ulikuwa ukilaumiwa na wataalam wa elimu.

Kauli hiyo imefuatia mwongozo ulioombwa leo Jumatano Februari Mosi, 2023 na Mbunge wa Bunda Vijijini (CCM), Mwita Getere.

Getere amesema kumekuwa na minong’ono kuwa kutotangazwa kwa mpangilio wa ufaulu kutadhoofisha elimu ya Tanzania.


“Kwa kuwa Serikali imo humu ndani kwanini isitoe taarifa humu ndani kipi bora. Hayo matangazo waliositisha yanaumuhimu gani kwa wananchi na yana ubora gani kwa wananchi,” amehoji.

Akijibu mwongozo huo, Profesa Mkenda amesema NECTA imeacha kupanga shule kwa ubora kutoka na sababu ya utata wa jambo hilo.

“Chukua shule ambayo inawatoto 100, nyingine ina wanafunzi 20, wamemaliza kidato cha nne, wanafunzi 170 wapata alama A, 30 hawakupata A, wenye wanafunzi 20 wote wamepata A kwa kuangalia wastani ufaulu ni wazi wenye wanafunzi 20 itatangazwa ni shule bora.

“Wengine watasema shule ya wanafunzi 70 wakapata A si bora zaidi, kuliko shule ya wanafunzi 20 tu. Ukiacha aina hiyo ya tathimini inaweka shinikizo kwa shule ya wanafunzi 100 kwa mfano kuhakikisha inawaondoa wale 30 waweze kutangazwa shule bora.”amesema.

Amesema kuwa kuna njia tatu zinaweza kutumika kufanya tathimini ikiwa ni pamoja na kuangalia matokeo ya mwisho ya mitihani kama iliyokuwa ikifanywa na NECTA.

Hata hivyo, amesema tatizo la njia hiyo haisemi shule imechangia nini katika maendeleo ya mtoto husika.

Amesema njia hiyo imeacha kutumiwa na nchi nyingi duniani na badala yake wanatumia nyongeza ya thamani (value edition) kwa kuangalia mwanafunzi alianza akiwa vipi na shule imechangia nini katika kumwinua mtoto katika masomo yake.


“Kwa maana hiyo shule bora inaweza kuwa ya kata tu, imechukua wanafunzi wanaoonekana wa wastani lakini wanapomaliza ile shule ikawa na matokeo mazuri kwa kuongeza ubora wa wanafunzi kuliko ile inayochagua wanafunzi bora tu,”amesema.

Amesema njia ya tatu si kwamba inaangalia mtoto aliingiaje shuleni bali na mazingira yake yakoje na kutolea mfano shule iko katika mzingira magumu maji hayapatikani karibu, hakuna mabweni na jamii masikini.

Amesema njia hiyo inaangalia japo mazingira hayo magumu lakini walimu wakafanya kazi na kuhakikisha mwanafunzi aliyeingia kwa wastani anapata daraja A.

Amesema katika mazingira hayo, shule hiyo itakuwa imeongeza kikubwa kuliko mwenye historia ya kuchukua wanafunzi mwenye ufaulu wa juu na katika mitihani yake ya mwisho akapata ufaulu mkubwa.

Amesema tathimini hiyo inahitaji wataalam wa takwimu na kwamba watakapokuwa na tathimini hiyo ndio wanaweza kuwaambia wazazi kuwa shule ipi ni bora.

Amesema kuwa hawajazuia mtu yoyote kusema shule ipi ni bora na kwamba matokeo yapo katika mtandao na Serikali haijaficha hilo.

“Lakini Serikali kupitia baraza halichukui kutangaza matokeo ambayo kisayansi yamelaumiwa na wataalam wa elimu. Lakini mbele baraza litaangalia namna nzuri ya kuzipangilia hizi. Hatuondoi ushindani na ndio maana tunaweka madaraja,”amesema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments