Tatizo la umeme Singida, Chongolo aahidi kuibana Serikali.


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ameahidi kuisukuma Serikali kuweka kituo cha kupoza umeme kati ya wilaya za Ikungi na Singida ili kupunguza adha ya kukatika kwa umeme na pia kusogeza umeme wa uhakika kwa wawekezaji.

Chongolo amebainisha hayo leo Jumanne, Februari 28, 2023 wilayani Ikungi mkoani Singida alipotembelea mgodi wa dhahabu wa Shanta ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake katika mkoa wa Singida akikagua utekelezaji wa ilani ya  chama cha mapinduzi ccm  mkoani Singida.

Akiwa katika mgodi huo, Chongolo amepokea changamoto kwa mwekezaji wa mgodi huo ambaye ni Kampuni ya Kitanzania ya Shanta Mining Co. Ltd kwamba wanahitaji kupata umeme wa uhakika kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za uchimbaji.

Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa kampuni ya Shanta, Honest Mrema ameomba kupatiwa umeme wa kutosha katika mgodi huo ili waweze kufanikisha malengo yao ya kuzalisha dhahabu kwa wingi.

"Tunaomba kupitia Tanesco kupatiwa umeme wa kutosha na wa uhakika kuendesha mitambo ya mgodi ili kupunguza matumizi ya mafuta kuzalisha umeme. Upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa uhakika unaweza kuiongezea Tanesco mapato ya Sh3 bilioni kwa mwaka," amesema.

Akizungumzia suala la umeme, Chongolo amesema amebaini wilaya za Ikungi na Manyoni zina changamoto ya umeme, hivyo anakwenda kuisukuma Serikali kuweka kituo cha kupoza umeme.

"Hili la umeme naomba mtuachie, tutakwenda kuisukuma Serikali kuweka kituo cha kupoza umeme karibu na wilaya za Ikungi na Manyoni," amesema Chongolo.

Amesisitiza kwamba ni muhimu Tanesco kuanza kujenga miundombinu ya umeme wa upepo ambao ni fursa kubwa kwa mkoa wa Singida ili kuongeza upatikanaji wa umeme kwa wananchi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments