TCRA kuzima laini za simu zisizohakikiwa kesho


 Wakati laini za simu ambazo hazijahakikiwa zikizimwa kesho Jumatatu Februari 13, 2023 na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), asilimia 96.8 ya laini zote za simu zilizosajiliwa kwa alama ya vidole zimehakikiwa. 

Hiyo ni kwa mujibu wa TCRA walipozungumza na Mwananchi huku wakieleza, hadi Februari 5, 2023, laini za simu 58.691 milioni zilikuwa zimehakikiwa kati ya laini milioni 60.620. 

Hiyo ikiwa na maana kuwa, idadi ya laini ambazo zilikuwa hazijahakikiwa zimepungua kutoka zaidi ya milioni mbili kwa mujibu wa TCRA zilizokuwapo Januari 19, 2023 hadi 1.92 milioni Februari 5. 

Takwimu hizo zinatolewa ikiwa ni baada ya Serikali kuongeza siku 14 mbele ili kutoa ruhusa kwa ambao walikuwa hawajahakiki laini zao ikiwa ni baada ya ukomo wa awali kuwa Januari 31, 2023. 

Akizungumza na Mwananchi Digital, Semu Mwakyanjala ambaye ni Ofisa Mwandamizi Mkuu Mawasiliano wa TCRA amesema usajili wa kutumia alama za vidole haukushindwa kudhibiti udanganyifu wa mtandao ila kinachofanyika sasa ni maboresho zaidi.

“Hadi Februari 5 laini za simu 58.691 milioni zilikuwa zimehakikiwa kati ya laini milioni 60.620 ambayo ni sawa na asilimia 96.8 Februari 5 mwaka huu, na kwa siku za hapo nyuma hadi leo (jana) idadi ya waliohakiki itakuwa imeongezeka,” amesema Mwakyanjala. 

Amesema kusajili laini kwa alama ya vidole ilikuwa kama njia ya kufungua vingi huku akieleza kinachofanyika sasa ni sawa na aliyenunua baskeli akaitumia kwa miezi mitatu na kuamua kuifanyia maboresho.

“Ukiamua kukagua nati gani imetoka kwenye baskeli siyo kwamba haifanyi kazi ila unataka uiendelee kuwa bora, ndiyo kinachofanyika,” amesema Mwakyanjala. 

Kuhusu laini ambazo zitafungiwa kama upo uwezekano wa watumiaji kuzirejesha (renew) alisema taarifa kamili itatolewa baada ya kukamilika kwa shughuli hiyo. 

Siku chache nyuma akitoa maelezo mbele ya waandishi wa habari, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema lengo la uhakiki ni kuendelea kudhibiti utapeli unaofanywa kwa njia ya simu. 

“Kumekuwa na utapeli mwingi kwa kutumia laini za simu, hatua ya awali ilikuwa ni usajili kwa alama za vidole na kila laini iliyokuwa imelengwa kusajiliwa ilisajiliwa,” amesema Nape na kuongeza. 

“Baadaye kampeni ya pamoja ya kuhakiki ilianzishwa na ilikubaliwa kuwa ambazo hazijahakikiwa zifungwe na 31 ilikuwa mwisho lakini tumeona tuongeze siku hadi Februari 13 mwaka huu. 

Kwa mujibu wa ripoti ya TCRA ya robo ya nne ya mwaka, hadi Desemba 2022 mitandao ya simu ilikuwa imesajili jumla ya watumiaji milioni 60.277. 

Watumiaji hao ni sawa na ongezeko la asilimia 4 ikilinganishwa na wale milioni 58.1 waliokuwapo mwisho war obo ya tatu ya mwaka 2022 yaani Septemba.

Kati ya watumiaji hao, Vodacom ilikuwa na jumla ya watumiaji milioni 18.18, Airtel watumiaji 16.61 milioni, Tigo milioni 15.94, Halotel milioni 8.02 na TTCL ikiwa na watumiaji 1.49 milioni huku Smile wakiwa na watu 15,547.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments